1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Onyo kali juu ya mabadiliko ya hali ya anga

Maja Dreyer6 Aprili 2007

Leo hii mjini Brussels, wataalamu wa masuala ya hali ya hewa kutoka nchi 120 wamekubaliana juu ya sehemu ya pili ya ripoti juu ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa. Mazungumzo yaliendelea hadi wakati wa usiku. Jambo kuu katika ripoti hii ni matokeo kwa wanyama na mimea yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/CB4s
Ongezeko la joto duniani linazidi kuleta athari
Ongezeko la joto duniani linazidi kuleta athariPicha: DLR

Sehemu ya pili ya ripoti ya halmashauri ya hali ya hewa duniani IPCC inayotolewa leo baada wiki moja ya mazungumzo mjini Brussels inafuatia sehemu ya kwanza ambayo ilichapishwa mwezi wa Februari. Wataalamu wa hali ya hewa wanaonya kwamba ongezeko la joto duniani litasababisha hasara kubwa na kwa haraka zaidi kuliko ilivyosemekana awali. Kwa ujumla ripoti hiyo ina urefu wa zaidi ya karasa 1400, lakini yaliyozusha majadiliano makali yalikuwa maneneo yaliyotumika katika muhtasari wa karasa 21 kwa ajili ya wanasiasa. Wanasayansi kadhaa waliwashutumu wajumbe wa serikali za Uchina, Urusi, Saudi Arabia na Marekani kwa kuhafifisha maonyo yao.

Ripoti hii inazungumzia athari kali sana pale inapotabiri uhaba wa maji unaweza kuwaathiri mabilioni ya watu, viumbe vya wanyama na mimea vitakwisha kabisa na kiwango cha maji ya bahari kitaongeza. Takriban asilimia 20 hadi 30 za viumbe vya mimea na wanyama vinatarajiwa kuwa katika “hatari iliyoongezeka” kufa ikiwa wastani ya joto duniani utazidi kwa nyuzi 1.5 hadi 2, ripoti inasema baada ya kufanyiwa marekebisha. Awali ripoti ilizungumzia “hatari kubwa” ya kuangamia viumbe hivi.

Wakati mazungumzo mjini Brussels yalikuwa bado yameendelea, waziri wa masuala ya maendeleo wa Ujerumani, Bibi Heidemarie Wieczorek-Zeul alitoa mwito kwa nchi za kiviwanda kuzisaidia zaidi nchi maskini katika kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Waziri alisema: “Jinsi sisi katika nchi za kiviwanda tunavyotengezea bidhaa yetu, jinsi tunavyotumia mazingira na nishati, ni kama kuuharibu na kuushambulia msingi wa maisha ya watu katika maeneo haya.”

Hapo, waziri Wieczorek-Zeul alimaanisha hasa bara la Afrika, nchi za Asia zenye maeneo makubwa ya mito kuingia katika bahari na mataifa madogo ya visiwa ya Pasifik. Kutokana na kuongezeka joto duniani, ripoti ya IPCC inasema mavuno ya mazao yatapungua sana. Kulingana na ripoti hii, nchi kadhaa za Kiafrika huenda zitalazimika zitumie asilimia 5 hadi 10 ya pato jumla la taifa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa. Waziri Wieczorek-Zeul anazitaka nchi za kiviwanda zipunguze utoaji wao wa gesi chafu kwa kiwango kikubwa.

Juu ya hayo alikuwa na pendekezo jingine. Ongezeko la joto duniani linasababishwa pia na kukatwa misitu mikubwa katika nchi za joto. Waziri huyu alisema: “Ninadai kuwa tuweke utaratibu wa msaada wa kifedha duniani ili kuzifidia nchi zinazoendelea kusimamisha kufyeka misitu. Kwa sababu nchi zinazoendelea ambazo zinahifadhi misitu hiyo, zinachangia kulinda hali ya hewa ya dunia nzima, na lazima zilipiwe fidia na jumuiya ya kimataifa.”

Halmashauri ya hali ya hewa duniani IPCC ilianzishwa mwaka 1988. Ripoti zake zinatumika kama msingi wa kisayansi kwa sera za kimataifa juu ya hali ya hewa.