Kesi ya Ongwen yaanza kusikilizwa ICC
6 Desemba 2016Ongwen anakabiliwa na mashitaka kadhaa ya mauaji, ubakaji na kuwatumia wanajeshi watoto wakati wa uasi wa kundi hilo. Kesi hiyo pia inafuatiliwa kwa karibu na wahanga wa uasi wa kundi hilo.
Ongwen ambaye sasa ana umri wa miaka 40 anakuwa askari wa kwanza wa zamani mtoto kushitakiwa katika mahakama hiyo kwa makosa 70 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu ambayo yalifanywa na kundi la waasi linaloongozwa na Joseph Kony.
"Uongozi wa LRA unajulikana ulimwenguni kote kwa ukatili wake dhidi ya Waafrika, lakini haijawi kutokea kamanda yoyote wa LRA kushitakiwa", anasema Elise Keppler kutoka shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch ambaye anaongeza kuwa kesi hiyo ni hatua moja muhimu.
Umoja wa Mataifa unasema kundi hilo liliwaua watu zaidi ya laki moja na kuwateka watoto elfu 60,000 tangu lilipoanzisha uasi wa umwagaji damu dhidi ya serikali ya Uganda.
Zaidi ya wahanga 4000 wanashiriki katika kesi ya Ongwen na maelfu wengine wanatarajiwa kufuatilia kesi hiyo kutokea kaskazini mwa Uganda kwa njia ya televisheni.
Waathirika wanauelezea ukatili wa kundi hilo hasa kwa kuwateka nyara vijana wadogo na kuwalazimisha kuwauma na kuwapiga marafiki na ndugu zao wa familia hadi umauti au kunywa damu yao.
Maisha ya Utoto
Akiwa mtoto Ongwen alitekwa na kupelekwa katika kundi na kisha kutumiwa kama askari mtoto. Lakini mwendesha mashitaka wa ICC amesema Ongwen alipokuwa mtu mzima aligeuka kuwa katili, na kuratibu utekaji nyara na utumwa wa "watoto chini ya umri wa miaka 15 walioshiriki kikamilifu katika uasi."
Ongwen anakabiliwa na mashitaka kadhaa ikiwemo ubakaji, mauaji, na "ndoa za kulazimisha", ikiwa ni kosa la kwanza kuwasilishwa katika mahakama ya ICC.
Wakati vijana wa kiume walifikia vyeo mbalimbali vya juu katika kundi hilo, vijana wa kike "walitumiwa kama nyara za vita" na watumwa wa ngono.
Ongwen anatajwa kuwa na wake saba, mmoja alikuwa na umri wa miaka 10 wakati alipobakwa. Kwa mujibu wa vipimo vya DNA, Ongwen amewazalisha wasichana kadhaa akiwa na jumla ya watoto 11.
Waendesha mashitaka wanadai pia kuwa kati ya mwaka 2002 na 2005, Ongwen alihusika na uvamizi huko kaskazini mwa Uganda ambapo aliamuru kuuliwa kwa raia waliokuwa katika kambi nne.
Waathirika wengi waliuawa katika vurugu, na walionusurika walikatwa midomo na masikio yao. Katika mojawapo ya kesi , shuhuda mmoja anasema Ongwen aliamuru vikosi vyake kupika na kuwala raia.
Upande wa Utetezi
Upande wa utetezi hata hivyo unasema unazingatia hoja kadhaa, kwamba Ongwen mwenyewe amekuwa akisumbuliwa na kiwewe cha mateso aliyoyapitia. Mawakili wake wanadai kuwa Ongwen alikuwa akifanya hayo chini ya shinikizo kwa kuwa aliishi katika kitisho cha kuuawa na Kony na makamanda wake.
Waendesha mashitaka wana nia ya kuwaleta mashahidi 74 wakiwemo askari wa zamani watoto pamoja na ushahidi mwingine ikiwemo mwasiliano ya simu, picha na vidio.
Hata hivyo wanaofuatilia kesi ya Ongwen wanaibua maswali ya kina namna ya kushughulikia kesi inayowahusisha watoto ambao walikabiliwa na unyanyasaji kwa miaka kadhaa kabla ya kugeuka kuwa wahusika wakuu. Kesi hiyo inawezekana ikiaacha historia ya kisheria.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef