1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ongezeko la deni la taifa lazusha mjadala Tanzania

Admin.WagnerD9 Novemba 2021

Wakati serikali ya Tanzania ikianisha jinsi itavyotumia mkopo wa zaidi ya shilingi trilioni 1.3, kutoka Shirika la fedha duniani  IMF, kumezuka hoja mpya kuhusu deni la taifa linalodaiwa kuendelea kuongezeka.

https://p.dw.com/p/42lOB
Ruanda | Samia Suluhu und Paul Kagame
Picha: Rwanda Presidency

Kiwango cha mikopo kilichoshuhudiwa katikia vipindi vyao vyote viwili vya marais Benjamin Mkapa na jakaya Kikwete na kile kipindi cha muhula mmoja cha Rais John Magufuli ndicho kilichoibua mjadala huo na kutokana na hali hiyo mbunge wa Mtama(CCM) Nape Nnauye ametaka kuanzishwe ukaguzi kubaini mwenendo huo.

Nape ambaye amewahi kuwa waziri katika serikali ya awamu ya tano na kudumu kwa kipindi kifupi kabla ya kutumbuliwa, anahoji kuwepo kwa ongezeko kubwa la deni katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.

Wachumi waonesha hofu ya athari ya mikopo mikubwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya nchi

Tansania Dar Es Salaam Kigamboni Brücke Hängebrücke
Daraja la Kigamboni, jijini Dar es Salaam TanzaniaPicha: Imago/Xinhua

Deni la taifa ni mjadala unaonekana kuvuta hisia za wengi hasa kutokana na kile kinachoelezwa kwamba huenda likawaweka katika njia panda walipa kodi. Licha ya serikali mara zote kusisitiza kuwa deni hilo linahimilika lakini hata hivyo, baadhi ya wanauchumi wanaonya kwamba ukopaji mkubwa wenye lengo la kugharimia miradi mikubwa kwa wakati mmoja inaweza kuleta mtikisiko kwenye mwenendo wa hali ya uchumi.

Na sasa kuibuliwa kwa hoja inayotaka kufanyika ukaguzi mahususi kuhusiana na deni hilo la taifa, kunavuta hisia nyingine kuhusiana na namna mikopo hiyo ya serikali na mchambuzi huyu, Majid Mjengwa amekuwa na haya ya kusema juu ya hayo yote yanayoendelea kuibuliwa wakati huu.

Deni hilo la taifa sasa limefikia kiasi cha shilingi trilioni 78

Deni hilo la taifa linalofikia kiasi cha shilingi trilioni 78, limegawika katika makundi mawili, yaani lile la ndani lenye thamani ya shilingi trilioni 18.23 na lile la nje likigharimu kiasi cha shilingi trilioni 59.69. Sehemu kubwa ya mikopo hiyo ni ile inayotumika kwa ajili ya uendelezaji wa miradi inayotekelezwa nchini ambayo mingine inagusa moja kwa moja huduma za kijamii.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi ambao wanatajwa ndiyo walipaji wa mikopo hiyo wamekuwa na hisia mseto juu ya kwa kama miradi hiyo inayotekelezwa inagusa moja kwa moja mahitaji yao, kama anavyoona mmoja wao huyo.

Hivi karibuni serikali  ya Tanzaniailipokea kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kutoka fuko la fedha la kimataifa IMF kama mkopo kwa ajili ya kupiga jeki maeneo ambayo yalianguka kutokana na janga la virusi vya corona. Serikali imeanisha namna fedha hizo zitakavyotumika.