1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ongezeko la bei za vyakula lasababisha vurugu nchini Somalia

Mwakideu, Alex5 Mei 2008

Polisi wamefyetua risasi na kuwauwa waandamanaji wawili

https://p.dw.com/p/Dtwa
Wasomali wanaubeba mwili wa mwenzao aliyeuwawa katika makabilianoPicha: AP

Watu wawili wamepigwa risasi na kuuwawa katika makabiliano ya polisi na waandamanaji waliogadhabishwa na ongezeko la bei za vyakula nchini Somalia.


Miongoni ya sababu zilizopelekea maandamano hayo ni kushuka kwa shilingi ya Somalia; jambo ambalo waandamanaji wanalala limesababishwa na baadhi ya wafanyibiashara wanaopendelea zaidi dola ya Marekani kuliko shilingi ya nchi hiyo.


Abdinur Farah alikuwa miongoni mwa waandamanaji hao na anasema alikuwa pamoja na mjombake kabla polisi kufyetua risasi na kumuua mjombake. Watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika makabiliano hayo.


Waandamanaji hao wakiwemo wanawake na watoto wamerusha mawe na kuvunja vioo vya magari na mabasi na kuwashambulia wenye maduka ambao baadaye walilazimika kufunga biashara zao.


Mfumuko wa bei nchini Somalia umepanda katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa miaka 17.


Watafiti wa Umoja wa Mataifa wanasema bei za bidhaa za nafaka zimepanda kwa kiasi cha asili mia 110 na 375 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wakati Somalia ya kati imeshuhudia ukame mkali.


Kwa sasa dola moja ya Marekani inabadilishwa kwa shilingi 25 elfu za Somalia ilhali mwaka wa 1991 wakati aliekuwa rais wa nchi hiyo Siad Barre alipong'atuliwa mamlakani dola ilikuwa ikibadilishwa kwa shilingi eflu nne.


Tangu wakati huo nchi hiyo imekuwa haina benki kuu ya kusimamia mfumuko wa bei.


Leo waandamanaji wamewashutumu wafanyibiashara kwa kuikataa shilingi yao wakisema kwamba hao sio wamarekani na kwamba wana pesa yao ya Somalia ambayo wangependelea kuitumia.


Kupungua kwa dola za marekani nchini humo kumepelekea kuundwa kwa noti za shilingi elfu moja bandia ambazo zimekuwa zikionekana sokoni kwa wingi.


Somalia iliondoa hela zingine zote na kubakisha noti hiyo ya elfu moja mwaka wa 2001 kufuatia kushuka kwa thamani ya pesa zake lakini jambo hilo halikuzuia mfumuko wa bei kupanda zaidi nchini humo.


Mire Hussein mkaazi mmoja wa Mogadishu anasema serikali haina fedha kwahivyo wafanyibiashara wengine wamekuwa wakitengeneza noti za elfu moja bandia huku wengine wakikataa kuchukua zile za zamani.


Wakaazi hao wanalaumu kuundwa kwa noti hizo bandia na wanasema huenda kukasababisha kuondolewa kwa shilingi ya Somalia na kuanzishwa kwa matumizi ya dola za marekani nchini humo.


Biashara ya simu za mkono, silaha na vyakula vya kawaida zimeufanya mfumuko wa bei nchini Somalia ubakie kawaida katika miaka kadhaa iliyopita.


Mapema wiki iliyopita Umoja wa Mataifa ulionya kwamba kupanda kwa mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Somalia kwa zaidi ya asilimia 100 katika kipindi cha miezi 15 iliyopita, kumesababisha ongezeko la bei za vyakula na kunatishia maisha ya mamilioni ya wasomali.


Takwimu za shirika la utafiti wa chakula katika Umoja wa Mataifa Food Security Analysis zinasema takriban wasomali milioni 2.6 wanahitaji msaada wa chakula kwa sasa hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 40 tangu January. Hali hii imesababishwa na mapigano ya mara kwa mara nchini humo pamoja na kuchelewa kwa msimu wa mvua uliokuwa uanze katikati ya aprili na juni.


Benki ya dunia imesema bei za vyakula imeongezeka mara dufu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita; jambo ambalo limesababisha ghasia nchini Misri na Haiti na maandamano nchini Brazil, India na vile vile Misri.


Miongoni mwa sababu zinazosababisha kupanda kwa bei ya chakula duniani ni matumizi ya nishati za mimea, vikwazo vya kibiashara, mazao duni pamoja na ongezeko la malipo ya usafirishaji.


Rais wa benki ya dunia Robert Zoelick amesema watu bilioni mbili kote duniani wanateseka kutokana na ongezeko hilo na wengine milioni mia moja katika nchi maskini wataishia kuwa maskini zaidi kutokana na tatizo hilo.


Shirika la chakula duniani WFP linahitaji dola milioni laki saba na hamsini na tano kwa dharura nalo shirika la chakula na kilimo FAO linapanga kutumia dola bilioni 1.7 kugawanya mbegu kwa wakulima masikini kama njia ya kuchangia mazao makubwa katika siku za usoni.