1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Oman yasema muafaka wa Yemen upo njiani

30 Machi 2021

Oman, ambayo ni mpatanishi kwenye mzozo nchini Yemen, inasema huenda makubaliano kati ya pande zinazohasimiana yakapatikana hivi karibuni kufuatia juhudi za pamoja kati ya nchi hiyo, Marekani na Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/3rOCA
Niederlande 2013 | Haitham bin Tariq Al Said, neuer Sultan von Oman (2020)
Picha: picture-alliance/dpa/Belga Photo/D. Waem

"Serikali ya Oman inatarajia kwamba mazungumzo haya yataleta matokeo yanayotazamiwa ili kurejesha amani na utulivu kwa ndugu zetu wa Yemen na pia kuimarisha usalama na maslahi ya nchi nyengine kwenye eneo hili." Ilisema taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la Oman (ONA) siku ya Jumanne (Machi 30).

Oman, ambayo ni jirani wa Yemen na Saudi Arabia, imekuwa ikiongoza jitihada za kimya kimya lakini kwa ushirikiano mkubwa na Saudi Arabia, Marekani na Umoja wa Mataifa, ili kufikia suluhisho la kisiasa kwa vita vya Yemen.

Baadhi ya maafisa wa kundi la waasi la Wahouthi, akiwemo kiongozi wa timu ya majadiliano Mohammed Abdulsalam, wamekuwa wakiishi nchini Oman tangu mataifa jirani kujiunga na vita vya wenyewe nchini Yemen mwaka 2015.

Saudi Arabia, ambayo inaongoza muungano wa kijeshi dhidi ya Wahouthi, ilitoa pendekezo la kusitisha mapigano wiki iliyopita, lakini Wahouthi wakasema ingelikubali tu pale mzingiro wa safari za anga na baharini ungeondolewa.

Jopo la Umoja wa Mataifa lawashutumu Wahouthi

Jemen Marib | Soldaten auf Truck
Wanajeshi wa serikalii inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kusini mwa Yemen.Picha: Ali Owidha/REUTERS

Huku hayo yakijiri, jopo la wataalamu cha Umoja wa Mataifa lilisema kuwa limegunduwa Wahouthi ndio waliohusika na mashambulizi ya tarehe 30 Disemba 2020 dhidi uwanja wa ndege wa Aden, ambayo yaliuwa watu 22 wakati wajumbe wa serikali inayotambuliwa kimataifa wakiwasili kusini mwa Yemen.

Jopo hilo la wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa lilisema kuwa wapiganaji wa Kihouthi walirusha makombora yao kuelekea uwanja wa ndege wa Aden kutokea maeneo mawili tafauti waliyokuwa wanayadhibiti, ambayo ni uwanja wa ndege wa Taiz na kituo cha polisi cha Dhamar.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia wawili ambao wanafuatilia kwa kina suala hilo, wataalamu hao waliwasilisha ripoti yao mbele ya Kamati Maalum ya Umoja wa Mataifa inayosimamia vikwazo dhidi ya Yemen tangu Ijumaa (Machi 27), lakini Urusi ikazuwia kuchapishwa kwake. 

Hata hivyo, Wahouthi waliikanusha ripoti hiyo iliyowasilishwa katika wakati ambapo utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani ukiwashinikiza waasi hao kukubali mpango wa amani, ambao unajumuisha pia usitishwaji mapigano.

Katika tukio jengine, jopo hilo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa limefuta tuhuma za ufisadi na utakatishaji fedha dhidi ya serikali, benki kuu na shirika moja lenye makao yake Umoja wa Falme za Kiarabu, likisema kuwa mapitio ya taarifa za awali hayakuguduwa ushahidi wowote.

Barua ya jopo hilo kwa kamati ya vikwazo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwa mkuu wa kampunji ya Hayel Saeed Anam ilisema kwa sasa inaondowa tuhuma hizo.