Olimpiki Rio:Afisa wa Kenya akamatwa
10 Agosti 2016Michael Rotich alikana shutuma zilizochapishwa katika gazeti la kila Jumapili la Times nchini Uingereza, ambalo lilisema kwamba alipigwa picha na waandishi habari ambao wanafanya uchunguzi wa chini kwa chini, wakijifanya ni wawakilishi wa wanariadha , miezi kadhaa iliyopita.
Kikosi cha timu ya Kenya kilimrejesha nyumbani Rotich, na alikamatwa jana Jumanne katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi wakati akiwasili kutoka Brazil na alipelekwa mahakamani.
Hajafunguliwa mashitaka, lakini polisi nchini Kenya imeomba awekwe kizuwizini kwa siku saba wakati inafanya uchunguzi zaidi. Anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani leo Jumatano baada ya kukamatwa usiku wakati akiwasili.
"Mtuhumiwa anashukiwa kufanya makosa kadhaa kinyume na sheria ya kupambana na madawa ya kuongeza nguvu misuli kwa wanamichezo yaani doping," Kirimi Muguna, afisa wa polisi anayehusika na masuala ya kupambana na biashara ya madawa ya kulevywa , alisema katika kiapo malum kilichowasilishwa mahakamani.
Historia ya mafanikio ya Kenya
Kenya nchi ambayo ina historia ya mafanikio katika mbio za masafa ya kati na marefu , heba yake imechafuliwa na hadi wanariadha 40 waliogunduliwa kutumia madawa hayo yanayoongeza nguvu misuli katika muda wa miaka minne iliyopita.
Mapambano yake kutaka kuwashawishi maafisa kwamba nchi hiyo inalichukulia suala hilo kwa dhati ilitishia timu ya Kenya kuondolewa katika kushiriki michezo ya Olimpiki ya Rio.
Rais wa Kenya mwezi Aprili mwaka huu alitia saini kuwa sheria mswada unaoelekeza kuwa ni kitendo cha uhalifu kutumia madawa hayo yaliyopigwa marufuku hali iliyotakiwa na shirika la kupambana na matumizi hayo la dunia ili kuepuka nchi hiyo kupigwa marufuku kushiriki katika michezo ya Rio.
Ni wiki iliyopita tu Kenya iliondolewa katika orodha ya mataifa yanayotumia madawa hayo yanayoonekana kukaidi sheria za shirika la kimataifa la kupambana na madawa hayo baada ya kuanzisha sheria hiyo mpya.
Ritich anachunguzwa na shirika la kupambana na madawa hayo nchini Kenya pamoja na uchunguzi wa kihalifu.
Chama cha riadha nchini Kenya kimekataa kutoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo.
Wanariadha wa Kenya pia wamepigwa marufuku kuzungumza na vyombo vya habari kuhusiana na suala hilo.
Kuogelea
Wakati huo huo michezo ya Rio inaingia katika siku yake ya tano, na jana muogeleaji Katie Ledecky amejinyakulia medali mbili za dhahabu kwa Marekani baada ya kushinda kuogelea kwa mita 200 na 400 mtindo huru, wakati pia Mmarekani Michael Phelps nae amenyakua medali mbili za dhahabu kwa kushinda mita 200 kuogelea mtindo wa kipepeo.
Na ndoto ya mchezaji maarufu wa tennis Serena Williams ya kunyakua medali yake ya tano ya dhahabu ya Olimpiki iliyeyuka jana wakati alipoondolewa katika mashindano hayo na mchezaji kutoka Ukraine Elina Svitolina kwa seti mbili kwa bila 6-4 na 6-3.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape
Mhariri: Mohammed Khelef