1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olimpiki: Mechi ya Afrika Kusini na Japan itachezwa?

19 Julai 2021

Michezo ya Olimpiki itakuwa inang'oa nanga huko Tokyo Japan kuanzia Ijumaa tarehe ishirini na tatu hadi Julai nane. Michezo hiyo imegubikwa na wingu la janga la virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3whHj
Japan Start olympischer Fackellauf
Picha: Du Xiaoyi/REUTERS

Mji unaoandaa michezo hiyo wa Tokyo unawekwa katika hali ya tahadhari kutokana na idadi kubwa ya maambukizi huku karibu thuluthi mbili ya raia wa Tokyo wakisema kamati andalizi ya Olimpiki haiwezi kudhibiti maambukizi michezo hiyo inapoendelea.

Katika taarifa inayofungamana na suala hilo ni kwamba timu ya kandanda ya Afrika Kusini haifahamu iwapo itacheza mechi yake ya ufunguzi dhidi ya Japan baada ya sheria za kuzuia maambukizi ya Covid 19 kupelekea wachezaji pamoja na makocha 21 kuwekwa karantini.

Waandalizi wa michezo hiyo ya olimpiki wamethibitisha kwamba waliokutana karibu na timu hiyo ya Afrika Kusini wamewekwa karantini. Masa Takaya ni msemaji wa kamati andalizi ya michezo hiyo ya Olimpiki Tokyo.

Masa Takaya, Sprecher des Tokioter Organisationskomitees
Msemaji wa kamati andalizi ya Olimpiki Masa TakayaPicha: DW/F. Lill

"Katika kundi hilo hilo watu watatu wameambukizwa virusi vya corona. Wachezaji na maafisa wao walitengwa mara tu walipogunduliwa kuwa wameambukizwa na wengine katika kikosi hicho wakatakiwa kusalia katika vyumba vyao na wanafuata masharti," alisema Takaya.

Ila swali walilokuwa wakijiuliza wengi ni iwapo mchezo wao dhidi ya Japan uliopangwa utaendelea.

"Bila shaka baada ya hapa kutakuwa na majadiliano na shirikisho la kimataifa na tutashirikiana na wahusika ili waendelee kushiriki mechi," alisema Takaya.