Olimpiki: Fainali ya mbio za mita 100 Jumapili
13 Agosti 2016Hatimaye michezo hiyo itashuhudia nafasi adimu ya kumuona binadamu anayekimbia kwa kasi duniani. Usain Bolt , bingwa mtetezi mara mbili wa mbio za mita 100 anaingia uwanjani kwa mara ya kwanza katika mbio za mchujo mchana leo. Fainali zitafanyika kesho Jumapili, na Bolt amewaambia wazazi wake yuko tayari kwa fainali hizo licha ya kuwa ana maumivu kidogo katika paja.
Fainali ya wanawake ya mbio za mita 100 itafanyika leo Jumamosi ambapo watachuana Elaine Thomson wa Jamaica, Murielle Ahoure wa Cote d'Ivoire, Dafne Schippers wa Uholanzi na Wamarekani English Gardner, Tianna Bartolette na Tori Bowie.
Tirunesh Dibaba wa Ethiopia tayari amenyakua medali ya shaba katika mbio za mita 10,000 mapema jana Ijumaa, sasa ni zamu ya mdogo wake Genzebe kuwania medali katika mbio za mita 1,500 leo. Genzebe bingwa wa dunia alifanikiwa kupita katika mbio za mchujo jana Ijumaa, na kuwaacha wapinzani wake kwa umbali mkubwa.
Neymar na Colombia
Katika soka robo fainali zimekwisha anza siku moja baada ya Sweden kuifadhaisha marekani kwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti kwa upande wa soka ya wanawake.
Pambano linalosubiriwa kwa hamu ni kati ya Brazil na Colombia kwa upande wa wanaume, ambapo pambano hilo lina hisia zake kufuatia pambano la robo fainali la kombe la dunia mwaka 2014 ambapo Juan camillo Zuniga wa colombia alipiga kigoti mgongoni Neymar na kuvunja mfupa wa mgongo.
Michezo mingine ni kati ya Ureno dhidi ya Ujerumani, Nigeria itaoneshana kazi na Denmark na Korea kusini dhidi a Honduras.
Kwa upande wa Tennis Mjerumani Angelique Kerber anawania dhahabu baada ya kuingia katika fainali dhidi ya Monica Puig wa Puerto Rico.
Super Cup
Kesho Jumapili nchini Ujerumani kutakuwa na pambano la kufungua msimu la kukata na shoka, ambapo mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich wanaikabili Borussia Dortmund iliyoshika anfasi ya pili katika ligi msimu uliopita katika Super Cup nchini Ujerumani.
Pambano hilo linaiweka Ujerumani nzima katika hamasa kubwa, ukitilia maanani kuhama kwa wachezaji muhimu kutoka timu moja kwenda nyingine.
Mlinzi na nahodha wa zamani wa Borussia Dortmund Mats Hummels amehamia kwa mahasimu wao na alikoanzia soka Bayern Munich , wakati mchezaji wa kati Mario Goetze amerejea kundini kutoka Bayern Munich akielekea katika timu alikokulia Borussia Dortmund.
Nako nchini Uhispania Barcelona wataingia dimbani kesho Jumapili kukabiliana na Sevilla katika pambano jingine la Super Cup nchini humo.
Premier League Uingereza
Wakati huo huo Ligi ya Uingereza Premier League inarejea uwanjani leo ambapo mabingwa watetezi wanaumana na Hull City , Everton wanawakaribisha makamu bingwa Tottenham Hot Spurs, na Manchester City wako nyumbani wakiikaribisha Sundeland.
Kesho Jumapili patachimbika wakati Arsenal itaikabili Liverpool , Bournemouth iko nyumbani ikiisubirin Manchester United na Chelsea inatiana kifuani na West Ham United.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef