1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hii ni mara ya nne kuwania urais tangu aingie katika siasa

25 Oktoba 2017

Wakati uchaguzi  wa marudio  ukitarajiwa kufanyika Oktoba 26, kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya,  Raila Odinga amesema hatashiriki uchaguzi huo. Hatua hiyo inatajwa kuwa itazima ndoto za kuwa rais wa nchi hiyo.  

https://p.dw.com/p/2mSBe
Kenia Raila Odinga bei Kundgebung in Mombasa
Picha: Reuters/J. Okanga

 

Badala yake, Odinga ameonekana kufanikiwa kurithi nafasi aliyoshika baba yake,  Jaramogi, Oginga Odinga. Ambaye aliongoza upinzani kwa miongo minne lakini si urais.

 Katika  uchaguzi  mkuu uliofanyika Agosti mwaka huu, Odinga alikuwa akiongoza  Muungano wa vyama vya upinzani, (NASA); huku akifanikiwa kuuondoa mgawanyiko  uliozoeleka baina ya vyama vya upinzani, kwa kile alichoona kuwa ni  mpango madhubuti wa kumshinda Rais Uhuru Kenyata 55, wa chama cha Jubilee.

Baada ya Kenyata kushinda, Odinga alilalamikia kuwepo kwa udanganyifu  na kupeleka malalamiko yake katika Mahakama Kuu nchini  humo. Mahakama ilitoa uamuzi  wa kushtua kwa kumpa Odinga ushindi nadra katika  nyanja za siasa.

Hata hivyo, Odinga, aliendelea mbele na kutaka Tume ya uchaguzi nchini humo ifanyiwe mabadiliko na baadaye aliamua kujiondoa katika kinyang´iro hicho , ikiwa ni wiki mbili kabla ya uchaguzi. Odinga alisisitiza kuwa  uchaguzi hautakuwa huru na wa haki.

 ``Kuna dalili  zote kuwa  uchaguzi wa tarehe 26  utakuwa mbaya kuliko wa awali,.`` amesema Odinga wakati alipotangaza kujiondoa.

  Odinga aliita tume ya uchaguzi kuwa ni kampuni ya uhalifu na akaongeza kuwa hatashiriki katika uvunjwaji huo wa sheria.

Kenyata na Odinga, wamekuwa ni mahasimu kuanzia katika ngazi ya familia  katika siasa za Kenya tangu wakati wa uhuru. Katika kizazi kilichopita, Jaramogi Odinga alishindwa kisiasa dhidi ya Jomo Kenyata, ambaye aliibuka na kuwa ni kiongozi wa kwanza wa taifa hilo baada ya uhuru.

Akiwa amezaliwa katika familia ya kisiasa,Odinga mtoto kutoka kabila la Luo, aliingia katika siasa wakati wa utawala wa Rais Daniel Arap Moi. Odinga aliwekwa kwa muda mrefu  gerezani  i kutokana na harakati za kupigania demokrasia.

 Alijaribu kuwania uraia bila mafaniklio mnamo mwaka 1997, 2007 na 2013 huku akidai kuwa ameibiwa kura katika vinyang´anyiro viwili vya mwisho, pamoja na kile cha mwaka huu mwezi Agosti.

Waangalizi wengi wanakubaliana na Odinga kuhusu madai yake, kuwa, uchaguzi wa mwaka 2007 uligubikwa na  kasoro.

 Uchaguzi wa 2007 uliosababisha machafuko bado ni jinamizi linaloziandama siasa nchini Kenya

Kenia | Proteste gegen den Wahlausgang vor dem Obersten Gerichtshof in Nairobi
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

 Uchaguzi huo  wa 2007, ndio uliosababisha machafuko ya kikabila yaliyowaacha zaidi ya watu 1,100 wakipoteza maisha. Ili kumaliza mgogoro huo, waangalizi wa kimataifa, walilazimisha mpango ambapo Mwai Kibaki aliendelea kuwa Rais na wakati huo Odinga, alichukua nafasi ya Waziri Mkuu  katika serikali ya Umoja wa Kitaifa.

 Alishika nafasi hiyo hadi mwaka 2013, ambapo aliwania tena urais na kushindwa na Uhuru Kenyata kwa tofauti ndogo sana ya kura huku akishindwa pia mahakamani alikokwenda kupinga matokeo.

Kwa mara nyingine tena, Odinga alilalamika kulikuwa na udanganyiku katika uchaguzi wa Agosti mwaka huu lakini safari hii, Mahakama Kuu, ilimpa ushindi na kufuta matokeo hayo kutokana na uvunjwaji wa sheria na kasoro mbalimbali.

 Baada ya muongo mmoja  tangu kutokea kwa machafuko ya 2007,  bado jinamizi linaziandama siasa za Kenya pamoja na changamoto za ukabila.

Wafuasi wa Odinga, miongoni mwao kabila la Waluo, wanaamini wananyimwa madaraka na kabila lenye idadi kubwa ya watu, la Wakikuyu  ambalo ni la Kenyata.

Odinga anadai kuwa uchaguzi wa haki utampa ushindi yeye na hata wafuasi wake wanaamini hivyo. Anasema Kenyata anajaribu kuvunja matakwa ya katiba mpya ya nchi hiyo huku akiiga tabia za kidikteta kama za  Rais wa zamani, Moi, ambao baba yake Odinga alipambana nao.

 Licha ya wafuasi wake kumtaja Odinga kuwa ni kiongozi atakayeleta mabadiliko, akitajwa kama mzungumzaji mwenye ushawishi mkubwa na anayeweza kuishawishi hadhara kwa hotuba zake, lakini pia anatajwa kuwa na sifa ya kuwa mkaidi na mwenye hasira za haraka.

Odinga amesomea uhandisi, zama za Ukomunisti, huko Ujerumani Mashariki; na alimpa mtoto wake mkubwa wa kiume,  jina la Fidel. Fidel castro alifariki mwaka 2015 wakati wa mapinduzi nchini Cuba.

Baada ya kurejea Kenya, mwaka 1970, Odinga alianza kwa kufanya biashara kabla ya kuingia katika siasa kama baba yake. Odinga ameowa na ana watoto watatu, Rosemary, Raila Junior na Winnie.

Mwandishi: Florence Majani

 Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman