Odinga asitisha maandamano yaliyoitikisa serikali ya Kenya
3 Aprili 2023Hatua hiyo inajiri baada ya Rais William Ruto kuafiki mapendekezo ya kuifanyia mageuzi Tume ya Uchaguzi kupitia mchakato utakaoongozwa na Bunge.
Tangazo la kusitishwa maandamano hayo ya upinzani lilitolewa siku ya Jumapili baada ya wajumbe wa makundi ya kidini na wanadiplomasia kukutana na kambi ya Raila Odinga na Rais William Ruto kwa nyakati tofauti kwa kipindi cha juma moja.
Huku kambi ya Raila ikitaka njia ya kusitisha maandamano hayo, kambi ya Rais Ruto imeshikilia kuwa haitaruhusu upinzani kujiunga na serikali kwenye mazungumzo hayo.
Miongoni mwa matakwa ya Upinzani ni kufanyiwa mageuzi mchakato wa kuwateua makamishna wa Tume ya Kusimamia Mipaka na Uchaguzi ya IEBC.
Upinzani wakataa makamishna wa tume kuteuliwa na jopo la rais
Tayari Rais Ruto alikuwa ameunda jopo la kuteua makamishna, hatua ambayo upinzani inataka ifutiliwe mbali.
Kwenye hotuba kwa taifa kwa njia ya televisheni, Rais Ruto ameonekana kulegeza msimamo wake wa awali huku akiuomba upinzani kuyakomesha maandamano.
"Napendekeza mazungumzo yatakayoongozwa na Bunge kuhusu suala la kuunda jopo la kuwateua makamishna wa IEBC kwa kuzingatia sheria na Katiba.”
Muda mfupi baada ya taarifa ya Rais Ruto kwa taifa, kiongozi wa upinzani Raila Odinga alitangaza kufutilia mbali maandamano akiitaja hotuba ya Rais kuwa yenye tija kwa maendeleo.
"Tunafutilia mbali maandamano tuliyokuwa tumeyapanga kufayika tarehe tatu Aprili, lakini tuna haki ya kuyaitisha iwapo mchakato huu hautazaa matunda.”
Awali Raila alikuwa ametangaza kuwa maandamano ya siku ya Jumatatu yangekuwa mabaya na makubwa. Raila akitoa masharti ya kuondelewa mashtaka kwa waandamanaji wote waliotiwa nguvuni.
Hoja ya ukali wa gharama za maisha bado ipo pale pale
Aidha upande wa Azimio unaitaka serikali kupunguza gharama ya maisha na kurejeshwa kwa makamishna wanne wa Tume ya IEBC waliojizulu baada ya kushinikizwa.
Huku akipuuza suala la makamishna hao, Rais alikuwa na haya ya kusemakuhusu gharama ya maisha.
"Tuna mpango kamili ambayo tunashughulikia gharama ya maisha. Kwa mara ya kwanza tumesajili wakulima milioni tano. Tumeagiza vyakula vya aina mingi.” amesema rais Ruto.
Majuma mawili yaliyopita Rais alisema kuwa hatakubali Raila kuvuruga taifa, hata hivyo usemi wake wa kulegeza msimamo umepongezwa na wengi.
Hatua ya kusitisha maandamano ni ahueni kwa wakenya wengi ambao shughuli zao zilikuwa zinavurugwa kila siku ya Jumatatu na Alhamisi huku serikali ikikadiria hasara ya shilingi bilioni tisa kwa majuma matatu ambayo maandamano hayo yameandaliwa katika miji ya Nairobi, Kisumu, Siaya na Migori.