1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Odinga apinga matokeo ya awali Kenya

Shisia Wasilwa9 Agosti 2017

Muungano wa upinzani NASA umekataa matokeo ya uchaguzi wa urais yanayomweka Rais Uhuru Kenyatta mbele ya mpinzani wake Raila Odinga. Odinga amesema matokeo hayo ni ya kughushi, akidai yeye ndiye anaongoza.

https://p.dw.com/p/2hvhY
Raila Odinga
Picha: Reuters/T. Mukoya

Kwa upande wao, chama cha Jubilee kimeonya upinzani dhidi ya kueneza kampeini za kuchochea wananchi dhidi ya matokeo hayo. Hadi tukienda mitamboni rais Uhuru Kenyatta alikuwa anaongoza kwa kura milioni 7.7 dhidi ya Odinga aliyekuwa na kura milioni 6.3. Tume ya kusimamia uchaguzi bado haijatangaza matokeo hayo rasmi.

Uchaguzi uliotarajiwa kuwa huru na wa haki nchini Kenya, sasa umeingiwa doa, baada ya muungano mkuu wa upinzani –NASA kudai kuwa chama cha Jubilee kimeshirikiana na Tume ya kusimamia uchaguzi kuwapoka ushindi. Matamshi hayo sasa yanaibua hali ya wasiwasi kwenye taifa ambalo lilitumbukia kwenye zogo mwaka 2007 ambapo watu zaidi ya1200 waliuawa na wengine laki tano kupoteza makazi, wakati upinzani ulipodai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki. Akiandamana na mgombea mwenza Kalonzo Musyoka na baadhi ya vigogo wa chama hicho, Odinga amewataka wafuasi wake kutulia wanapofikiria hatua watakayochukua. "Mataokeo haya si ya kweli, ukiyatazama utagundua kuwa hayabadiliki, kuna mbinu ambayo inatumika, mpinzani wangu amekuwa akiongoza tangu mwanzo hadi mwisho. Tunao ushahidi wa kuthibitisha,” amesema Odinga.

Kura zahesabiwa Kenya
Kura za uchaguzi mkuu zahesabiwa KenyaPicha: Reuters/T. Mukoya

Kiongozi wa muungano mkuu wa upinzani akionekana kuwa mwenye hasira, Odinga amedai kuwa mitambo ya tume ya kusimamia uchaguzi ya kupeperusha matokeo ilizimwa na kisha kukarabatiwa kuonesha kuwa rais uhuru Kenyatta anaongoza. Odinga aliongeza kusema kuwa kufuatia ukarabati huo, matokeo hayo yameathiri kaunti 37 kati ya kaunti 47. Kwa mujibu wa takwimu alizozitoa mwenyewe, Odinga amedai kuwa matokeo halisi yanaonyesha yeye ana kura milioni 8.1 huku Kenyatta akiwa na milioni 7.2. Amesema kuwa nia ya wananchi lazima izingatiwa na kuwa rais lazima aondoke mamlakani na tume ya kusimamia uchaguzi iwajibike. "Matokeo tunayopata ni ya jumbe fupi, ambayo hayako kwenye sheria. Form 34 hazistahili kuja baada ya matokeo, zinastahili kuambatana na matokeo.”

Kwa upande wao, chama tawala kupitia katibu wake Raphael Tuju kimeuonya upinzani dhidi ya matamshi ambayo yanaweza kulitumbukiza taifa kwenye hali ya taharuki. Tuju anadai kuwa mawakala wa uchaguzi wa upinzani wanastahili kujitokeza na kuthibitisha fomu za kupigia kura. "Kwamba tumeshinda lakini ushindi wenyewe utatangazwa na IEBC, lazima tutii sheria,” ameeleza Tuju.

Hadi Jumatano mchana tume ya kusimamia uchaguzi haikuwa imetoa tamko lake kuhusu madai ya muungano mkuu wa upinzani. Kwa sasa hali imetulia japo kuna hali ya taharuki. Hayo yanajiri huku waangalizi wa uchaguzi huu wakisema kuwa walikuwa wameridhika na maandalizi ya asasi zote zilizokuwa zinahusika na uchaguzi huu.

 

Mwandishi: Shisia Wasilwa, DW, Nairobi

Mhariri: Iddi Ssessanga