Obama ziarani katika bara la Ulaya
23 Mei 2011Rais wa Marekani Barack Obama, akianza ziara ya mataifa manne barani Ulaya nchini Ireland leo, amesema kuwa anataka kuhimiza biashara baina ya mataifa hayo na atafanya kila anachoweza kusaidia kuufufua uchumi wa Ireland. Obama pia ametembelea kijiji wanakotoka mababu wa upande wa mamake katika kijiji cha Moneygall.
Kwa Ireland , ziara ya Obama na ile iliyofanywa na malkia Elizabeth wiki iliyopita, ni kitu kinachokubalika ili kuyaondoa macho ya dunia katika kuangalia tu vurumai la matatizo ya kiuchumi nchini humo. Obama pia ataizuru Uingereza, Ufaransa na Poland katika ziara ya wiki nzima ambapo atajadili na viongozi wenzake masuala kama ya Afghanistan na Pakistan baada ya kuuwawa kwa kiongozi wa kundi la al-Qaeda Osama bin Laden, masuala ya uchumi wa dunia pamoja na mabadiliko yanayotokea katika mataifa ya kiarabu.
Akizungumza baada ya kuwa na mazungumzo na waziri mkuu wa Ireland, Enda Kenny, Obama amesifu uhusiano wa karibu kati ya Marekani na Ireland na kueleza kuridhishwa kwake na hatua za kuuimarisha uchumi wa Ireland. Kitu ninachosisitiza ni kwamba tunataka kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na biashara kati ya nchi zetu, na kwamba tutaweka juhudi za kuuimarisha uchumi wa Ireland.
Obama anatarajiwa kutoa hotuba muhimu kwa mamia wa watu wa mjini Dublin katika tukio litakalofanyika katika eneo la wazi, huku kukiwa na ulinzi mkali.
Ikulu ya Marekani imesema kuwa rais Barack Obama atatangaza baraza jipya la pamoja la usalama pamoja na Uingereza wakati akiwa nchini Uingereza wiki hii. Wasaidizi wa Obama wanasema kuwa juhudi hizo zitasaidia nchi hizo mbili kufanya kazi kwa pamoja na kubadilishana taarifa za kijasusi katika masuala ya muda mrefu yanayoleta changamoto, hususan katika mashariki ya kati na Afghanistan.
Kabla ya ziara yake hii Obama alizungumzia kuhusu hali ya ushirikiano ilivyo kati ya Marekani na bara la Ulaya.
"Nafikiri katika miaka saba au minane iliyopita, kumekuweko hali ya mgongano baina ya Marekani na mataifa ya Ulaya. Na moja kati ya malengo ya serikali yangu ni kujenga upya ushirikiano huu wa kihistoria."
Ziara hii ya Obama pia itamfikisha nchini Uingereza, katika mkutano wa kundi la nchi za G8 nchini Ufaransa na pia Poland , ikilenga zaidi kuhusu Afghanistan, pamoja na operesheni za NATO nchini Libya , na pia mjadala juu ya kiongozi mpya wa shirika la fedha la kimataifa, IMF.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri : Othman Miraji