Obama ziarani India.
8 Novemba 2010Katika mkutano wake na Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, Rais wa Marekani Barack Obama, aliielezea India kama taifa lenye nguvu duniani na kusema kuwa nchi zote mbili zitafanya kazi pamoja kuimarisha amani duniani.
Amesema anamatumaini kuwa katika majadiliano yake pamoja na, Waziri Mkuu, Rais na viongozi wengine wa India wataendelea kuuujenga zaidi uhusiano wao wa kibiashara ambao tayari wanao na kuimarisha zaidi ushirikiano katika masuala ya uchumi kati ya nchi hiyzo mbili na kimataifa.
Obama aitetea Benki kuu ya nchi yake:Aidha Rais Obama amefahamisha kwamba kukua kwa asilimia ndogo au kutokukua kabisa kwa uchumi wa Marekani hakutakuwa na manufaa yoyote na kutasababisha athari kwa uchumi wa dunia.
Ametoa ufafanuzi huo kufuatia hatua ya benki kuu ya nchi yake, kukosolewa na nchi nyingine juu ya uamuzi wake wa hivi karibuni, ambapo inataka kununua dhamana ya mipango ya muda mrefu ya serikali kwa ajili ya kujaribu kushusha kiwango cha riba kwa mikopo ya nyumba na madeni mengine kwa ajili ya kuhimiza utoaji wa mokopo na kusaidia ukuaji wa uchumi.
Hatua hiyo ilikosolewa na Waziri wa Uchumi wa Ujerumani kwa kusema kuwa inaongeza kutokuwa na uhakika katika uchumi wa dunia.
Suala hilo linatarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa kundi la nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi G20, utakaofanyika Korea Kusini baadaye wiki hii.
Obama na Singh wazungumzia ugaidi:Aidha katika mkutano wao wa pamoja viongozi hao walikubaliana juu ya nchi zao kufanyakazi kwa karibu zaidi kupambana na ugaidi duniani pamoja na uzuiaji wa uenezaji wa silaha za nyuklia.
Aidha Rais Obama pia aliishukuru India kwa mchango wake inayotoka katika mapambano dhidi ya ugaidi na harakati za kuirudisha Afghanistan katika mikono salama, kutoka kwa wapiganaji.
Rais wa Marekani anakamilisha ziara yake leo ya siku tatu nchini India ambapo pia amepangiwa kukutana na viongozi wa serikali na wapinzani, pamoja na kulihutubia bunge la India.
Awali alipotembelea mji wa Mumbai, alitangaza makubaliano ya biashara yenye thamani ya dola bilioni 10 ambayo yatasaidia kupatikana kwa ajira zipatazo 50, 000 nchini Marekani.
Obama kutembelea nchi nyingine za Asia:Katika ziara yake ya siku 10 barani Asia, Rais wa Marekani atazitembelea pia Indonesia, Korea kusini na Japan, ambapo pia anatarajiwa kushinikiza kupata ufumbuzi kwa hali ya kutokuwepo usawa katika masuala ya fedha duniani, suala atakalolipa kipaumbele katika mkutano wa viongozi wa mataifa ya G-20 utakaofanyika mjini Seoul, Korea Kusini.
Mwandishi Halima Nyanza(dpa, Reuters, afp.ap)
Mhariri: Josephat Charo