1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ziarani Berlin na Syria magazetini

19 Juni 2013

Ziara ya rais Barack Obama wa Marekani mjini Berlin, mkutano waG8 na siku 200 za kiongozi mpya wa kanisa katoliki ulimwenguni, ni miongozi mwa mada zilizopewa kipaumbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani .

https://p.dw.com/p/18srH
Rais Barack Obama akutana na kansela Angela Merkel katika ofisi ya kansela mjini BerlinPicha: Johannes Eisele/AFP/Getty Images

Tuanzie Berlin ambako rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kuwahutubia wageni zaidi ya elfu sita katika uwanja wa Paris katika lango mashuhuri la Brandenburg. Gazeti la "Thüringische Landeszeitung linaandika:"Anaweza kutamka maneno ambayo yatakuwa na umuhimu mkubwa ulimwenguni.Mwanasiasa huyo ambae tayari anabebeshwa jukumu la kuhusika na vita vya mtandao,anaweza kuonyesha tuzo ya amani ya Nobel ameistahiki na kutilia mkazo fikra ya kuwepo amani ulimwenguni.Bila ya shaka hotuba pekee haitoigeuza dunia kuwa bora.Lakini maneno mazuri humtoa nyoka pangoni kwa hivyo maneno yanaweza kuleta mabadiliko.Panahitajika fikra tu ya aina bora ya kuishi pamoja,la sivyo hali itaendelea kama ilivyo,hisia za kutoaminiana zitazagaa,upelelezi utazidi sawa na vita dhidi ya ugaidi."

Uhusiano kati ya Marekani na Ujerumani nao pia umechambuliwa. Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linaandika:"Uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani umeingia ufa.Sababu za hali hiyo ziko nyingi tu.Kwanza kuna ile hali kwamba Obama binafsi amewavunja moyo wengi kati ya wananchi wa Ujerumani.Halafu watu hawajasahau kiburi cha wamarekani walipoamua peke yao kuingilia kati kijeshi nchini Iraq,kuna hata wale wanaonung'unika kuhusu kuendewa kinyume haki za binaadam pia.Zaidi ya hayo kuna kizazi kipya hivi sasa ambacho hakishukurii mchango wa wamarekani dhidi ya utawala wa wanazi au vita baridi katika wakati ambapo Marekani kwa upande wake inadhihirisha hivi sasa kutaka kuelemea zaidi upande wa mataifa yanayopakana na bahari ya Pacific badala ya atlantik.

Msimamo wa Ujerumani umepata nguvu

G8 Gipfel in Nordirland 18.06.2013
Viongozi wa mataifa manane tajiri kiviwanda: kutoka juu :waziri mkuu wa Uingereza David Cameron,rais Barack Obama wa Marekani,rais Francois Hollande wa Ufaransa,waziri mkuu wa Canada Stephen Harper,waziri mkuu wa Italia Enrico Letta,rais wa baraza la Ulaya Herman Van Rompuy,mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Manuel Barroso,waziri mkuu wa Japan Shinzo Abbe,kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: Reuters

Mkutano wa kilele wa mataifa manane tajiri kiviwanda mjini Enniskillen huko Ireland Kaskazini umechambuliwa kwa marefu na mapana na wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Syria iligubika sehemu kubwa ya mazungumzo anasema mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine" na kuendelea:"Mkutano huo wa kilele uligubikwa na ahadi za kuhamakisha za kuendelea kutuma silaha nchini Syria.Wale walioamaini kwa dhati wangeweza kumtanabahisha rais Vladimir Putin asiusaidie kijeshi utawala wa Bashar al Assad,wangebidi wao wenyewe kwanza wasitangaze wanataka kuwapatia silaha waasi.Upande huo serikali kuu ya Ujerumani imefanya la maana ilipopinga kuwapatia asilaha waasi.Msimamao wa kansela Angela Merkel umepata nguvu huko Enniskillen.Na kwa namna hiyo Ujerumani inaweza kukabidhiwa jukumu la upatanishi na kuepusha mivutano kati ya rais Barack Obama na kiongozi mwenzake wa Urusi Vladimir Putin."

Kishindo kinachomkabili Papa Francis

Papst Franziskus in Vatikan 12.06.2013
Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa FrancisPicha: Reuters

Na hatimaye gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika kuhusu siku 200 tangu kiongozi mpya wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis wa kwanza, alipochaguliwa."Papa anahisi kwamba mtu anaweza kuwa na madaraka bila ya kulazimika kuyatumia. Anatambua kwamba anawatia kishindo baadhi waliozowea maisha ya raha katika uongozi wa kanisa.Anatambua pia akichokoza mambo,jibu halitakawia.Kwa hivyo awamu ya pili ya siku 100 za uongozi wa Papa Francis itakuwa ngumu na pengine muhimu pia."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo