Obama, Xi wamaliza mkutano wao
9 Juni 2013Marais hao walitumia saa nane pamoja katika muda wa siku mbili, katika makundi ya yaliyokuwa na ukaribu ya wafanyakazi, katika chakula cha jioni, pamoja na kutembea katika bustani nzuri katika eneo lililotunzwa vizuri katika jangwa la Califonia.
Ilikuwa mkutano wa kwanza kati ya China na Marekani tangu Xi mwenye umri wa miaka 59 kuchukua madaraka kamili ya nchi hiyo Machi na Obama mbunifu wa kupanga upya diplomasia ya Marekani kuelekea bara la Asia ambaye anatazamwa kwa jicho la shaka shaka na China, kuchukua madaraka katika kipindi cha pili cha utawala wake.
Pande zote mbili zilitaka kulegeza mazungumzo hayo kati ya China na Marekani kuwa ya kawaida, na hali hiyo imeonekana kufanikiwa. Katika wakati fulani Obama na Xi , wakitafuta msimamo wa pamoja kama wanasiasa , walitayarisha mitazamo yao katika kuelekeza kule ambako wanataka kuyaelekeza mataifa yao.
Masuala nyeti
Wakati Xi alipoondoka jana jumamosi(08.06.2013), maafisa wa Marekani wamesema , viongozi hao wawili walizungumza moja kwa moja kuhusu maeneo ya matatizo, usalama katika mtandao, wakashutumu mkwamo kuhusu mpango wa kinuklia wa Korea ya kaskazini na kukubaliana kuhusu msukumo mpya wa pamoja kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.
Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani Tom Donilon amesema mazungumzo hayo , yalikuwa kabisa si rasmi , ya maana na yaliyozungumzia mambo mengi na yenye mwelekeo mzuri kwaajili ya uhusiano muhimu wa mataifa hayo mawili yenye nguvu duniani , ambao mara nyingi umekuwa katika hali ya mivutano na ulihitaji ukarabati wa kila mara.
Kansela wa taifa wa China Yang Jiechi amesema viongozi hao hawakuona haya kuelezea tofauti zao, ikiwa ni pamoja na mauzo ya silaha ya Marekani kwa Taiwan na madai ya China ya maeneo katika bahari ya kusini mwa China.
Hawakuoneana haya
Obama na Xi wamekubaliana kufanyakazi kwa pamoja kuwezesha kuzuwia silaha za kinuklia katika rasi ya Korea, kufuatia majaribio ya kinuklia na makombora pamoja na onyo kali la vita vya silaha za atomic vilivyotolewa na korea ya kaskazini , mshirika mkubwa wa China ambae huleta usumbufu mkubwa.
Wamefanikiwa kupata kwa kiasi kikubwa msimamo wa pamoja katika suala hilo, Donilon amesema , na amesifu hatua za hivi karibuni zilizofikiwa na China kumpuuzia kimya kimya kiongozi wa Korea ya kaskazini ambaye hana uzoefu Kim Jong-Un.
Obama wakati huo huo ameweka wazi kuwa wimbi la mashambulizi ya China dhidi ya Marekani katika mtandao katika haki miliki ya biashara nchini Marekani pamoja na teknolojia ya kijeshi, litakuwa suala linaloleta utata katika uhusiano baina ya mataifa hayo.
Donilon amesema kuwa Xi , alikiri kuwa suala hilo ni muhimu kwa Marekani, na aliondoka Califonia akiwa hana shaka kuhusu wapi Obama anasimamia katika suala hilo.
Viongozi hao pia wametoa mwongozo kwa makundi ya maafisa kutoka kila nchi ambao wanatarajiwa kukaa chini na kujadili suala la udukuzi katika mtandao wa internet mwezi Julai.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Bruce Amani