Obama na Putin watofautiana kuhusu hatma ya Assad
29 Septemba 2015Katika hotuba zao tofauti katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa hapo jana, Rais Obama amemtaja Rais wa Syria Bashar al Assad kama kiongozi wa kiimla anayewaua watoto huku Putin akisema ulimwengu unapaswa kumuunga mkono Assad katika kupambana na wanamgambo wenye itikadi kali wa dola la kiislamu IS na kuonya ana mipango ya kuimarisha misaada ya kijeshi kwa utawala wa Assad.
Baada ya hotuba zao katika mkutano huo mkuu wa Umoja wa Mataifa, Obama na Putin walikutana kwa mkutano wa ana kwa ana uliodumu dakika tisini ambapo pia walikubaliana kuwa majeshi yao yanapaswa kufanya mazungumzo ili kuzuia mkwaruzano kati yao kwani majeshi yote yanafanya kampeini za kijeshi nchini Syria.
Putin aahidi kuendelea kumuunga mkono Assad
Marekani, Ufaransa na nchi washirika zinafanya mashambulizi ya angani dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS ambao wamechukua fursa ya kuwepo msukosuko nchini humo na kuyadhibiti maeneo makubwa Syria na Iraq.
Baada ya mkutano huo, Rais Putin amewaambia wanahabari kuwa nchi yake inafikiria ni njia zipi zaidi zinaweza kuisadia serikali ya Syria na wapiganaji wa kikurdi kupambana dhidi ya IS na kuongeza kuna fursa ya kufanya kazi kwa pamoja na Marekani kushughulikia tatizo hilo la IS.
Kiongozi huyo wa Urusi hata hivyo amesema sio wajibu wa Marekani au Ufaransa kuamua ni nani anastahili kuwa kiongozi wa Syria kwani hilo linaweza tu kuamuliwa na wasyria wenyewe.
Obama kushirikiana na Urusi kupambana dhidi ya IS
Rais Obama kwa upande wake amesema yuko tayari kushirikiana na Urusi na hata Iran kuvimaliza vita vya Syria ambavyo vimedumu zaidi ya miaka minne ambapo zaidi ya watu laki mbili wameuawa na mamilioni ya wengine wameachwa bila ya makaazi lakini hakubaliana na pendekezo la kusalia madarakani Rais Assad kwani yeye ndiye mhalifu mkubwa zaidi wa mzozo wa Syria.
Obama hakutaja moja kwa moja kuondolewa madarakani Assad na badala yake amedokeza kuwa kunaweza kuwa na kile alichokitaja kipindi cha mpito hiyo ikiwa dalili ya hivi karibuni kuwa Marekani inazingatia kumuacha Assad kusalia madarakani kwa muda, mtizamo ambao unazingatiwa na nchi za Umoja wa Ulaya.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande na waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu wamepinga uwezekano wa Assad kuruhusiwa kusalia madarakani.
Waziri wa mambo ya nje wa Qatar Khalid al Attiya ameionya Urusi kuwa imeshindwa kushughulikia chanzo cha mzozo wa Syria ambacho anasema "ni utawala wa Assad." Putin na Obama pia waliuzungumzia mzozo wa Ukraine katika mkutano wao, suala ambalo limesababisha hali ya vita baridi kati yao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp/dpa
Mhariri: Hamidou Oummilkheir