1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na Putin wataka mapigano yasimamishwe Syria

19 Juni 2012

Rais Barack Obama wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi wamekubaliana kwamba umwagaji damu nchini Syria lazima ukomeshwe, lakini hawakupendekeza hatua mpya za ufumbuzi wa mgofgoro huo wala kuodosha tafauti zao.

https://p.dw.com/p/15HzA
Rais Vladimir Putin wa Urusi (kushoto) na Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Vladimir Putin wa Urusi (kushoto) na Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: Reuters

Wakati hali ya umwagaji damu ikizidi kuwa mbaya nchini Syria na ikiwa ni wiki moja kufuatia kulaumiana kwa mtindo wa wakati wa Vita Baridi kati ya Marekani na Urusi,mazungumzo hayo hapo jana wakati wa Mkutano wa Kilele wa Kundi la G20 wa nchi tajiri na zile zinazoinukia kiuchumi duniani ulikuwa kama ni mtihani kuona iwapo Obama na Putin wanaweza kuwa na uhusiano wa kuweza kufanya kazi kwa pamoja.

Lakini viongozi hao wawili inaonekana kwamba hawakubaliani kwa mambo mengi juu ya hatima ya Rais Bashar al -Assad na mkutano wao huo wa ana kwa ana haukuashiria matumaini.

Huo ni mkutano wao wa kwanza tokea Putin arejee kwenye wadhifa wa urais mwezi uliopita na viongozi hao walikuwa wakitaka kujadili mizozo juu ya kuipatiwa silaha serikali ya Syria na uwezekano kwa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua zaidi dhidi ya serikali hiyo.

Obama amewaambia waandishi wa habari, baada ya mazungumzo hayo ambayo yalichukua zaidi ya masaa mawili kuliko vile ilivyokuwa imepangwa, kwamba wamekubaliana juu ya haja ya kukomeshwa kwa umwagaji damu na kuanzishwa mchakato wa kisiasa kuzuwiya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Majadiliano kuendelea

Kwa upande wake Putin amesema kutokana na maoni yake wamekubaliana juu ya vipengele vingi kuhusu suala hilo la Syria na kuongeza kwamba pande hizo mbili zitaendelea na majadiliano.

Mashambulizi katika mpaka wa Syria na Uturuki.
Mashambulizi katika mpaka wa Syria na Uturuki.Picha: DW/G.Anderson

Tafauti kati ya pande hizo mbili zilipamba moto wiki iliopita wakati Waziri wa Mambo ya nchi za Nje wa Marekani Hilary Clinton alipoituhumu Urusi kuwa inaupatia utawala wa Assad helikopta za kivita.

Mazungumzo hayo yamekuja wakati vikosi vya usalama vya Syria vikiendelea kushambulia kwa mizinga maeneo yanayokaliwa na upinzani nchini kote Syria. Mashambulizi makubwa ya mizinga yameripotiwa kutokea katika mji wa Douma ilioko kama kilomita 15 kutoka mji mkuu wa Syria ambao kwa wiki kadhaa umekuwa kwa kiasi fulani ukidhibitiwa na waasi ambao wamejiunga katika uasi dhidi ya Assad.

Vikosi hivyo pia vimekuwa vikiendelea kushambulia ngome kuu za waasi katika mji wa kati wa Homs na Damascus.

Mauaji zaidi Syria

Kituo cha Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria kimesema watu 94 wameuwawa nchini kote hapo jana wakiwemo raia 63,wanajeshi watatu walioasi na wanajeshi 28 wa serikali.

Kiongozi wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Robert Mood.
Kiongozi wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Robert Mood.Picha: dapd

Wakati huo huo habari kutoka Moscow mji mkuu wa Urusi zinasema kwamba ili kuhakikisha usalama wa raia wake,Urusi inajiandaa kuepeleka meli zake mbili za kivita katika bandari ya Tartus nchini Syria ambapo nchi hiyo ina kambi ya wanamaji.

Shirika la habari la Interfax limemkariri afisa mmoja katika makao makuu ya wanamaji wa Urusi akisema kwamba meli hizo The Nikolai Filchenkov na The Tzezar Kunikov zinapangwa kupelekwa katika bandari hiyo ya Tartus zikiwa na idadi kubwa ya wanamaji

Meli hizo mbili zinaweza kubeba wanajeshi 1,500 pamoja na silaha vikiwemo vifaru n,mizigo na zana nyenginezo.

Kusitishwa kwa shughuli za waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria mwishoni mwa juma kumeongeza shinikizo kwa Obama na Putin kuchukuwa hatua haraka kuzuwiya mzozo huo kugeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Mohamed Dahman/ RTR /AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman