1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na Jintao kukutana kwa mazungumzo leo

Halima Nyanza19 Januari 2011

Rais Barack Obama leo atakutana kwa mazungumzo na Rais wa China Hu Jintao mjini Washington, ambaye yuko huko kwa ziara ya siku nne. Mazungumzo yao yatazingatia masuala mbalimbali hususan ya uchumi na usalama.

https://p.dw.com/p/zzXu
Rais Barack Obama wa Marekani akiwa na Rais wa China Hu JintaoPicha: AP

Rais Barack Obama atamkaribisha baadaye leo mgeni wake Rais wa China Hu Jintao katika Ikulu ya nchi hiyo kwa heshima zote za kijeshi, kabla ya kuanza mazungumzo yatakayojadili masuala mbalimbali ambayo bado nchi hizo mbili hazijakubaliana ikiwemo sera ya sarafu, masuala ya haki za binadamu na mitazamo tofauti katika Asia.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Msemaji wa Rais wa Marekani, Robert Gibbs amesema wataendelea kuwa na mazungumzo mazito na akifafanua zaidi yale yatakayojadiliwa katika mkutano wa viongozi hao.

Rais Obama na Rais Jintao pia wanatarajiwa kujadili kwa kina juu ya madai ya Marekani  kwamba China inaitunza sarafu yake ya Yuan kuonekana kuwa ipo katika ngazi ya Chini jambo ambalo ni la kinafiki, ili kuweza kuimarisha bidhaa zake inazozisafirisha nje ya nchi hiyo.

Wa Marekani wengi wamekiwa wakiilaumu China kwa ongezeko kubwa la watu wasiokuwa na ajira nchini humo na kwamba wabunge wa nchi hiyo  wamekuwa wakishinikiza kuwepo sheria dhidi ya sera ya sarafu ya China, ambayo wanasema inatoa upendeleo katika kuwasaidia wataalamu wa China.

Aidha, wachambuzi wa mambo wanasema viongozi wote Obama na mwenziye Jintao  katika mkutano wao huo pia watajaribu kupunguza hali ya kutoaminiana kati ya pande hizo mbili.

Viongozi hao wawili wanatarajiwa pia kuijadili Korea kaskazini na mradi wake wa nyuklia.

Baada ya mazungumzo yao viongozi hao wawili pia watakutana na viongozi wa wafanyabiashara wa Marekani na China.

Na katika mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika katika Ikulu ya Marekani, Rais Jintao pia anatarajiwa kukabiliana na maswali juu ya rekodi ya haki za binadamu ya China na kifungo kinachomkabili sasa mrithi wa Rais Obama wa tuzo ya amani ya Nobel, mpigania demokrasia Liu Xiaobo.

Rais Jintao aliwasili jana nchini Marekani na kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 12, Rais wa Marekani leoa atamuandalia dhifa ya kitaifa kwa mgeni wake huyo katika Ikulu ya nchi hiyo.

Ziara hiyo ya Rais Jintao mjini Washington, imeelezwa kuwa mwanzo mpya wa uhusiano kati ya China na Marekani. Na kwamba ziara hiyo inafanyika wakati Marekani ikihangaika kuimarisha uchumi wake wakati China ikiongeza nguvu yake kiuchumi.

Na katika hatua nyingine, mamia ya wanaharakati wa haki za binadamu, walikudanyika jana, karibu na Ikulu ya nchi hiyo, huku wakipaza sauti kuitaka China iachane na mauaji na kuliachia huru jimbo la Tibet.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp, Reuters)

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed