1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na Castro wapeana mikono

11 Aprili 2015

Rais Raul Castro wa Cuba na Rais Barack Obama wa Marekani wamepeana mikono na kuzungumza kwa muda katika mkutano wa kilele wa mataifa ya Amerika mjini Panama.

https://p.dw.com/p/1F6DJ
Barack Obama und Raúl Castro reichen sich die Hand
Rais Raul Castro (kulia)akipeana mkono na rais Barack Obama(shoto)Picha: Reuters

Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wa Marekani na Cuba kwa pamoja kuhudhuria mkusanyiko rasmi tangu kuvunja uhusiano wao mwaka 1961.

Viongozi hao wawili walikutana na kusalimiana hapo Ijumaa (10 Aprili) wakati wakikusanyika pamoja na viongozi kutoka eneo hilo kabla ya sherehe za ufunguzi wa mkutano huo, amesema msemaji wa baraza la usalama la taifa la Marekani, Bernadette Meehan.

Eröffnung des Amerika-Gipfels in Panama
Viongozi wa mataifa ya America katika picha ya pamojaPicha: Getty Images

Mkutano huo ni wa kwanza kwa Cuba kualikwa kushiriki katika mkutano wa kimkoa, na macho yote yalielekezwa kwa Castro wakati akiwasili.

Castro alikuwa akitabasamu na kuzungumza na rais wa Panama Juan Carlos Varela na mkewe kabla ya kujiweka katika nafasi yake miongoni mwa viongozi wa eneo hilo, ambao walisimama katika mistari mitatu mbele ya bendera za mataifa hayo.

Gwaride la watoto

Uzinduzi huo uliochukua saa nzima , ulioongozwa na watoto wawili wanaowakilisha hali ya baadaye ya mataifa hayo, na pia ulishuhudia hotuba za kuwakaribisha iliyotolewa na Varela, katibu mkuu wa mataifa ya America Jose Miguel Insulza, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na ujumbe kutoka kwa kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis.

Viongozi hao baadaye walishuhudia gwaride la watoto wakivalia nguo maalum zinazovaliwa na wenyewe wa mataifa hayo yanayoshiriki katika mkutano huo, waliongozwa na bendi ya polisi waliovalia sare nyekundu.

Obama und Castro zum Auftakt des Amerika-Gipfels in Panama
Rais Castro na Obama wakisalimiana na viongozi wengine katika mkutano huo wa kilelePicha: Reuters

Chakula maalum kwa ajili ya viongozi hao ambapo tukio hilo si rasmi lilifuatia sherehe hizo za ufunguzi. Tukio hilo la kupeana mikono ni ishara ya hivi karibuni kabisa ya mjongeleano tangu Obama na Castro mwishoni mwa mwaka jana kukubaliana kuanzisha njia ya kurejesha uhusiano.

Leo Jumamosi (11.04.2015)unapangwa mkutano wa kihistoria ambapo viongozi hao watakutana ana kwa ana.

Tangu mapinduzi ya Cuba na kutaifishwa kwa makampuni yaliyokuwa yakimilikiwa na Marekani katika kisiwa hicho cha Karibiki, kumekuwa hakuna uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo ambazo zinatenganishwa na ujia wa maji wa kilometa 180 baina yao.

Wapinzani wa Cuba

Mapema jana Ijumaa (10.04.2015) Obama amekutana katika meza ya duara na wapinzani wa Cuba kama sehemu ya jukwaa la vyama vya kijamii, hali inayoonyesha mgawanyiko ndani ya nchi hiyo hata wakati akijitayarisha kujenga daraja la uhusiano mwema na rais Castro.

"Wakati Marekani inaanza ukurasa mpya katika historia na Cuba , tunamatumaini utajenga mazingira ambayo yanafanya kuwa bora maisha ya watu wa Cuba," amesema.

UN General Sekretär Ban Ki Moon in Bagdad
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-MoonPicha: picture-alliance/dpa/Karim Kadim

"Mataifa imara hayahofu wananchi wake wakakamavu. Mataifa imara yanakumbatia na kusaidia kuwawezesha wananchi wake wakakamavu," ameongeza.

Marekani imeweka uhakika wa haki za binadamu nchini Cuba kuwa kitu muhimu katika hatua ya kukaribiana na Havana.

Cuba kwa upande wake , inasisitiza kutaka kuondolewa katika orodha ya Marekani ya mataifa yanayodhamini ugadi kabla ya kuanza kupiga hatua katika mchakato huo.

Wakati huo huo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amewasifu marais Barack Obama na Raul Castro kwa kuelekea katika kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baada ya miongo kadhaa ya uhasama.

Ban amesema katika mkutano wa mataifa ya America kwamba eneo hilo "linafikisha mwisho mgawanyiko wa muda mrefu kwa njia ya kihistoria , kama tunavyoona katika chumba hiki."

Tukio la kihistoria

Amedokeza kwamba ni mara ya kwanza kwa mataifa yote 35 ya bara la America kuhudhuria mkutano huo. Cuba ilitengwa kwa miaka mingi, na Ban amesema kuwapo kwa rais Raul Castro jioni ya siku ya Ijumaa inatimiza matakwa yaliyokuwa yakihisika katika eneo lote.

Ban amesema hii ni hatua ambayo inalingana na mkataba wa Umoja wa Mataifa na "lengo lake la kuhimiza ujirani mwema."

Nguvu za nyota ya kiongozi wa kanisa Katoliki papa Francis zinahisika katika mkutano huo wa mataifa ya America.

Vatikan Karfreitag Papst Franzislus betet Kreuzweg am Kolosseum
Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa FrancisPicha: Reuters/Alessandro Bianchi

Katika ujumbe uliosomwa na waziri wa nchi wa kanisa hilo lenye makao yake makuu Vatican Pietro Parolin , kiongozi huyo mkuu wa kanisa Katoliki wa kwanza kutoka mataifa ya America ya kusini amewataka viongozi kutafuta msimamo wa pamoja kutatua matatizo yanayolikumba eneo hilo lenye wakatoliki wengi.

Kiongozi huyo wa kidini mzaliwa wa argentina amesema kwamba hata wakati mataifa ya America ya kusini yamepiga hatua kiuchumi katika miaka ya hivi karibuni , idadi kubwa ya watu wanaendelea kuishi katika umasikini na kupunguza pengo kati ya walionacho na wasio kuwa nacho kutakuja tu wakati serikali zitakapochukua hatua madhubuti.

Mwandishi: Sekione Kitojo/dpae/ape
Mhariri: Mohammed Khelef