1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na Cameron wazidi kuzibana Iran, Syria

15 Machi 2012

Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, wakubaliana kuongeza shinikizo dhidi ya Syria na Iran na kusaidia Afghanistan kiusalama kabla ya kuondoka kwa majeshi ya kigeni mwaka 2014.

https://p.dw.com/p/14KvL
Rais Barack Obama (kushoto) na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.
Rais Barack Obama (kushoto) na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.Picha: AP

Katika kikao chao cha pamoja na waandishi wa habari mjini Washington viongozi hao wamezungumzia mpango wa nyuklia wa Iran na pia kumuonya Rais wa Syria Bashar Al -Assad juu ya athari zinazoweza kutokea ikiwamo matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi yake endapo ataendelea na vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu, hasa mauaji ya wapinzani wake

Rais Obama ameionya serikali ya Iran kuwa wigo wa kushughulikia masuala ya Iran kidiplomasia unazidi kupungua na kuishauri iyatazame mapatano yajayo na mataifa yenye nguvu duniani kwa jicho la umakini wa hali ya juu na kusema kuwa bado matumizi ya nguvu za kijeshi yanachukua nafasi kubwa katika kutatua mzozo huo huku Cameron akiunga mkono msimamo huo.

Hakuna uharaka wa kuondoka Afghanistan

Wakiwa katika Ikulu ya Marekani viongozi hawa pia walijadili kuhusu vita vya Afghanistan huku wote wakipinga mpango wa kujiondoa haraka kwa majeshi ya kigeni nchini humo hususan baada ya mauaji ya raia 16 wa Afghanistan yaliyofanywa na mwanajeshi mmoja wa Marekani.

President Barack Obama and British Prime Minister David Cameron hold a joint news conference in the East Room of the White House in Washington, Tuesday, July 20, 2010. (AP Photo/Charles Dharapak)
Viongozi wa Marekani na Uingereza wakizungumza na waandishi wa habariPicha: AP

Kura za maoni zinaonesha kuwa hali ya kupinga ushiriki wa nchini hizo katika vita vya Afghanistani baina ya wananchi wa mataifa hayo imeongzeka jambo ambalo Rais Obama na chama chake cha Democrats wanaliona kama turufu inayoweza kuwapotezea ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2012

Hata hivyo, viongozi hao wameonesha imani ya ushirikiano wao huku kila mmoja akimtazama mwenziwe kama msaidizi muhimu katika kufikia malengo waliyoyapanga katika vikao vyao mbalimbali nchini Marekani. Obama amemuelezea Cameron kama rafiki muhimu huku Cameron naye akimuelezea Obama kama kiongozi mwenye busara.

Kuhusu mpango wa NATO nchini Afghanistan, viongozi hao wameweka wazi kuwa kwa sasa wanataka kujikita katika nia ya kurejesha jukumu la ulinzi wa taifa hilo katika mokono ya Waafghan wenyewe ifikapo mwaka 2013 na dhamira ya kuondoa majeshi yao ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014.

Pamoja na hayo, Rais Obama amewatoa hofu Waafghan kuwa wakati huu hawatafanya mabadiliko yoyote ya ghafla ya kuondoa majeshi na kwamba mambo yatakwenda kama yalivyopangwa. Aidha, mkutano wa NATO utakaofanyika mwezi Mei mwaka huu ndio utakaojadili kwa kina kuhusu suala hilo.

Mwandishi: Stumai George/AFP/REUTERS
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman