1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama, Mfalme Salman waijadili Iran, IS

Mohammed Khelef28 Januari 2015

Ujumbe mzito wa Rais Barack Obama wa Marekani kwenda kutoa pole kwa ufalme wa Saudi Arabia baada ya kifo cha Mfalme Abdullah unatajwa kuwa kipimo kwa diplomasia iliyoathirika ya mataifa hayo mawili.

https://p.dw.com/p/1ERxn
Rais Barack Obama wa Marekani (kushoto) na mwenyeji wake, Mfalme Salman wa Saudi Arabia.
Rais Barack Obama wa Marekani (kushoto) na mwenyeji wake, Mfalme Salman wa Saudi Arabia.Picha: Reuters/J. Bourg

Mara tu baada ya kukutana na mgeni wake, Mfalme mpya Salman al-Saud alituma ujumbe kwenye akaunti yake ya Twitter, akisema kwamba lilikuwa ni jambo la fahari kukutana na Rais Obama, akiongeza kwamba wawili hao walijadili "mafungamano ya kihistoria na ushirika wa kimkakati" kati ya nchi zao katika kuunga mkono amani ulimwenguni.

Lakini kile ambacho Mfalme Salman hakukitaja kuwa kiligusiwa kwenye mazungumzo yao ni rikodi ya haki za binaadamu ya Saudi Arabia, ambayo daima Marekani imekuwa ikisema ina mashaka nayo, ingawa haijawahi kufika umbali wa kutoa matamko ya kulaani vitendo vya ukandamizaji wa serikali dhidi ya raia.

Maafisa wa Marekani walisema Obama alilizusha suala hilo kwa njia ya jumla jamala bila kugusia mkasa wa mwandishi wa blogu, Raef Badawi, ambaye amehukumiwa kuchapwa viboko 1,000 kwa kile ambacho mamlaka za Saudia zinasema ni kuukashifu Uislamu. Adhabu hiyo, ambayo sasa imesitishwa kwa sababu za kiafya, imezusha wasiwasi mkubwa kwenye jamii ya kimataifa.

Iran, Dola la Kiislamu kwenye ajenda

Kwa mujibu wa mashirika ya habari ya kimataifa, Rais Obama na Mfalme Salman waliutumia mkutano wao kujadiliana pia suala la programu ya nyuklia ya Iran, nchi ambayo Saudi Arabia inaichukulia kama adui yake mkubwa kwenye Ghuba ya Ajemi.

Kutoka kulia: Mfalme Salman wa Saudi Arabia, Rais Barack Obama wa Marekani na mkewe, Michelle.
Kutoka kulia: Mfalme Salman wa Saudi Arabia, Rais Barack Obama wa Marekani na mkewe, Michelle.Picha: Reuters/J. Bourg

Hata hivyo, sehemu kubwa ya mazungumzo ilijikita kwenye operesheni ya kijeshi inayoongozwa na Marekani dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq, ambayo Saudi Arabia ni mshiriki wake tangu ilipoanza mwaka jana.

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Marekani aliyemo kwenye msafara huo alisema viongozi hao wawili walikubaliana kuendelea kuwasaidia wapinzani nchini Syria na pia haja ya kuimarisha umoja wa kitaifa nchini Iraq.

Saudi Arabia ina wasiwasi kwamba kusambaa kwa nguvu na ushawishi wa kundi hilo la Dola la Kiislamu kunaweza kuiathiri moja kwa moja.

Kundi hilo lilitoa mkanda wa vidio mara tu baada ya kifo cha Mfalme Abdullah wiki iliyopita, likishangiria kifo cha yule waliyemuita "Abdullah katili" na kuapa kwamba wataivamia Saudi Arabia hivi karibuni.

Katika picha hii cha mwaka 2010, Rais Barack Obama wa Marekani na mgeni wake, Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, kwenye Ikulu ya Marekani.
Katika picha hii cha mwaka 2010, Rais Barack Obama wa Marekani na mgeni wake, Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, kwenye Ikulu ya Marekani.Picha: picture-alliance/dpa/Roger L. Wollenberg/abaca

Shaka za Saudi Arabia kwa Marekani

Lakini wachambuzi wanasema Saudi Arabia imekuwa hairidhishwi na namna ambavyo Marekani inajitenga na mizozo iliyopo kwenye nchi nyengine za Kiarabu kama vile Yemen na Libya na badala yake imekuwa ikielemea sana upande wa Asia.

Obama ameongoza ujumbe wa watu 29 kutoka vyama vyote viwili vikuu vya kisiasa nchini Marekani, wakiwemo maafisa wa utawala wa zamani wa George Bush, wote wakisema walitaka kuonesha kuunga kwao mkono uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia.

Taifa hilo la Kiarabu ni mzalishaji mkubwa wa mafuta, ambayo sehemu yake kubwa huchimbwa na kutumia na kampuni za Marekani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga