1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama Kuzuru Saudi Arabia

Lilian Mtono/AFPE/EAP15 Aprili 2016

Rais wa Marekani, Barack Obama wiki ijayo atamtembelea Mfalme Salman wa Saudi Arabia na viongozi wengine mjini Riyadh ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kurekebisha mahusiano hasi kati ya nchi hizo mbili zinazofungamana

https://p.dw.com/p/1IWgi
USA Saudi-arabischer König Salman bei Barack Obama
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Kabla ya kuchaguliwa kuwa rais, Obama aliwahi kupuuzia ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, na tangu hapo kumekuwepo na mahusiano ya wasiwasi mkubwa kati yao katika vipindi vyote viwili vya utawala wa Obama.

Ingawa ziara hiyo inayotarajiwa kuwa siku ya Jumatano ikiwa ni ya nne kwa kiongozi huyo katika ufalme wa Saudia, Wasaudi wenyewe wamekuwa wakichukizwa na ushiriki wake juu ya Iran na uungaji wake mkono katika kukabiliana na machafuko kwenye baadhi ya nchi za Kiarabu.

Pamoja na kwamba nchi hizo zinaungana katika kukabiliana na kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu, IS, kwa upande mwingine, Saudi Arabia inaamini kwamba Obama angeweza kuwa na ushawishi wenye nguvu zaidi, dhidi ya Rais wa Syria, Bashar al-Assad, kuliko Urusi iliyochukua jukumu hilo.

Kutohudhuria kwa Mfalme Salman katika mkutano wa nchi za Ghuba ulioitishwa mwaka jana na Rais Obama nchini Marekani, kuliibua maswali mengi juu ya mahusiano ya nchi hizo, ingawa mshauri mwandamizi wa rais Obama Rob Malley alisema tangu wakati huo kumekuwepo na hatua kubwa iliyofikiwa katika kuboresha mahusiano kati ya viongozi hao.

Marekani na Saudia zapania kuimarisha mahusiano

Malley amesema, katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kumekuwepo na mikutano ya mara kwa mara katika ngazi tofauti kuzungumzia masuala ya usalama. Na katika ziara hiyo inayoanza Jumatano, baada ya kusalimiana na Mfalme, Obama na Salman watakutana na viongozi wa Baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba, GCC linalotawaliwa na Saudia na kuaminika kuwa na nguvu kubwa zaidi katika ukanda huo.

Baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba,GCC
Baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba,GCCPicha: AFP/Getty Images/F. Nureldine

"Kumekuwepo na ushirikiano wa kina kati yetu na GCC" amesema Malley akiangazia juhudi za kukabiliana na machafuko ya kikanda nchini Libya na Yemen. "Bado kuna mengi yanayohitaji kufanyika, ingawa nchini Yemen, hali ni shwari zaidi ikilinganishwa na mwaka uliopita" alisema Malley, huku akizungumzia hatua ya kusitisha mapigano nchini Yemen iliyoanza kutekelezwa jumapili iliyopita.

Obama kwenda Uingereza na Ujerumani

Obama anatarajiwa kuondoka Riyadh usiku wa Alhamisi ijayo, na kuelekea nchini Uingereza na baadae Ujerumani. Hata hivyo ikiwa imesalia wiki moja kwa kiongozi huyo wa Marekani kuanza ziara hiyo, serikali ya nchi hiyo imeendelea kutoa hadhari kwa raia wake wanaotaka kusafiri kwenda Saudi Arabia, kwa madai ya kuwepo kwa taarifa za vitisho dhidi ya raia hao na wengine wa Ulaya na maeneo mengine yenye ushirikiano na nchi hizo.

Taarifa hiyo ya hadhari, inayofuatia ile ya awali iliyotolewa mwezi Septemba mwaka jana, inaonya kwamba makundi ya kigaidi ya Al-Qaeda na Dola la Kiislamu, IS, kwa pamoja wanajipanga kufanya matukio ya uvamizi katika maeneo hayo, huku maeneo yanayolengwa yakiwa ni mahoteli, migahawa, maeneo ya maduka, shule za kimataifa na maeneo mengine ambayo watu wa Ulaya hukutana.

Aidha, hadhari hiyo inawaonya maafisa wa Marekani kutokaribia eneo la mpaka wa Yemen kwa zaidi ya Kilomita 80, na kuwataka Wamarekani kubaki hotelini na maeneo yao ya makaazi.

Katika ziara yake hiyo, Obama ambaye pia atazuru Uingereza, anatarajia kutumia muda wake mwingi nchini akiwa nchini humo. Amepangiwa kukutana tena na Malkia Elizabeth wa Pili kwa chakula cha mchana katika kasri la Windsor, siku ya Ijumaa ikiwa ni siku moja baada ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa ya Malkia Elizabeth, ambaye atakuwa ametimiza miaka 90.

Malkia Elizabeth wa 11
Malkia Elizabeth wa 11Picha: picture-alliance/dpa/PA

Katika hatua nyingine, Obama atakutana na Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, anayepigania nchi yake kubaki ndani ya umoja wa Ulaya, EU. Waingereza wanatarajia kupiga kura ya maoni ya ama kubaki au kujitoa kwenye jumuiya hiyo itakayofanyika mwezi Juni mwaka huu.

Hata hivyo, Obama hatarajiwi kuzungumzia chochote kuhusiana na kura hiyo ya maoni, ingawa wapambe wake wanaunga mkono Uingereza kubaki ndani ya Umoja wa Ulaya. "Ataweka wazi kuwa suala hili ni la waingereza wenyewe kufanya maamuzi wakati wa kupiga kura mwezi Juni" amesema Ben Rhodes, mshauri msaidizi wa masuala ya usalama wa kitaifa, alipozunguza na waandishi wa habari kuhusiana na ziara hiyo.

Mwandishi:Lilian Mtono/afpe

Mhariri:Saumu Yusuf