1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama kuwafuata 'Dola la Kiislamu' hadi Syria

Mohammed Khelef11 Septemba 2014

Huku Marekani ikikumbuka mwaka wa 13 tangu mashambulizi ya Septemba 11, Rais Barack Obama ameidhinisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya "Dola la Kiislamu" nchini Iraq kuvuka mpaka kuingia Syria.

https://p.dw.com/p/1DADM
Rais Barack Obama wa Marekani akihutubia taifa juu ya hatua za nchi yake dhidi ya kundi linalojiita "Dola la Kiislamu."
Rais Barack Obama wa Marekani akihutubia taifa juu ya hatua za nchi yake dhidi ya kundi linalojiita "Dola la Kiislamu."Picha: Reuters

Katika mkesha wa kumbukumbu za mashambulizi yaliyoibadilisha historia ya kutokushambuliwa kwa taifa kubwa kabisa duniani, kiongozi wa taifa hilo ameapa kwamba sasa atawaangamiza wanamgambo wanaojiita "Dola la Kiislamu" kwa kuwa wamekuwa kitisho kwa Marekani na maslahi yake.

"Nimesema wazi kwamba tutawasaka magaidi wanaoitishia nchi yetu, popote walipo. Hilo linamaanisha kwamba sitasita kuchukuwa hatua dhidi ya waasi wa Dola la Kiislamu nchini Syria, na pia Iraq. Huo ndio msingi muhimu wa urais wangu: ukiitisha Marekani, hutakuwa na mahala pa kujificha," alisema Rais Obama kwenye hotuba yake kwa taifa.

Kauli hii ya Obama sasa inaashiria kuwa mtazamo wake kuelekea mzozo wa Syria unabadilika. Hotuba hii imekuja wiki mbili tu, baada ya kukosolewa vikali kwa kauli yake kwamba Marekani haina mkakati wowote dhidi ya waasi hao nchini Syria, na miezi sita baada ya kutangaza kuwa kundi hilo halikuwa na nafasi kubwa kwenye mzozo huo.

Syria bila Assad?

Bado maafisa wa serikali ya Marekani hawajasema lini mashambulizi hayo yataanza, ingawa tayari Marekani imekuwa ikiwashambulia wanamgambo hao ndani ya Iraq kwa kile inachosema ni kutokana na mualiko wa serikali ya Iraq.

Mtu anayejitambulisha kuwa kiongozi wa kundi la "Dola la Kiislamu", Abu Bakr al-Baghdadi.
Mtu anayejitambulisha kuwa kiongozi wa kundi la "Dola la Kiislamu", Abu Bakr al-Baghdadi.Picha: picture alliance/AP Photo

Hata hivyo, kwa Syria, Marekani itapaswa kufanya mashambulizi bila ya ruhusa kutoka kwa Rais Bashar al-Assad kwa kuwa inamchukulia kiongozi huyo kuwa si halali. Afisa mmoja wa Marekani amesema Saudi Arabia imekubali kufungua vituo vya mafunzo kwa ajili ya makundi ya waasi wa Syria wenye msimamo wa wastani, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha kukabiliana na kitisho cha wanamgambo wanaojiita "Dola la Kiislamu".

Rais Obama ameliomba bunge la nchi yake kuidhinisha mpango huo wa kuwapa mafunzo na silaha waasi wa Syria, lakini Spika wa Congress, John Boehner, amemkosoa Rais Obama kwa kushindwa kuelezea mkakati wa kuliangamiza kundi la "Dola la Kiislamu" kwa haraka.

Boehner anayetokea chama cha Republican amesema pendekezo la Obama la kuwapa mafunzo na silaha waasi wa Syria, litachukua miaka kadhaa kabla ya kutekelezwa kikamilifu.

Upinzani Syria waikaribisha hotuba ya Obama

Muungano wa upinzani wa Syria umeukaribisha mpango huo wa Obama, ingawa umetaka hatua kali zaidi dhidi ya Rais Assad. Katika taarifa waliyoitoa hivi punde kufuatia hotuba hiyo ya Obama, Muungano huo umeliomba Bunge la Marekani kuidhinisha mpango wa dola milioni 500 kuwasaidia waasi kupambana na Assad, ukisema ndiye mzizi wa kukua na kusambaa magaidi wa Dola la Kiislamu.

Mwakilishi wa Muungano wa Upinzani wa Syria, Louay Safi.
Mwakilishi wa Muungano wa Upinzani wa Syria, Louay Safi.Picha: cc-by-nc-nd/UN Photo/Jean-Marc Ferré

Sambamba na kuwafuata wanamgambo wa Dola la Kiislamu nchini Syria, Obama amesema pia kwamba nchi hiyo itaongeza msaada wake kwa wanajeshi wa Iraq na Kurdistan, ikiwemo kuongeza wanajeshi wengine takribani 500, ambao watakuwa na jukumu la kutoa mafunzo na vifaa na ukusanyaji wa taarifa za kijasusi.

"Tutaongeza msaada wetu kwa wanajeshi wanaopambana na magaidi kwenye medani ya kivita. Mwezi Juni, nilituma wanajeshi kadhaa Iraq kutathmini kile tunachoweza kufanya kulisaidia Jeshi la Iraq. Sasa timu hizio zimekamilisha kazi yao na Iraq imeunda serikali, tutatuma wanajeshi wengine 475 nchini Iraq. Kama nilivyosema kabla, wanajeshi hawatashiriki vita vya ardhini. Hatutaburuzwa tena kwenye vita vyengine nchini Iraq," alisema Obama.

Bunge la Marekani linajitayarisha kumpigia kura mpango huo wa Rais Obama dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu, ambao licha ya kuonesha kuungwa mkono na umma, wabunge wa chama cha Republican wanautilia shaka kwa kutokuwa na uwazi wa kutosha.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga