1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama kutoa heshima kwa wahanga wa utawala muovu Argentina

Admin.WagnerD24 Machi 2016

Rais wa Marekani Barack Obama akiwa anaendelea na ziara yake nchini Argentina, atatoa heshima ya kuwakumbuka wahanga wa utawala muovu wa kijeshi ulioungwa mkono na Marekani miaka 40 iliyopita.

https://p.dw.com/p/1IIfM
Argentinien Barack Obama und Mauricio Macri in Buenos Aires
Picha: Reuters/C. Barria

Wiki hii Argentina inatimiza miaka 40 tangu kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1976 yaliyouweka madarakani utawala wa wanajeshi kwa zaidi ya miaka saba ambao bado unaiandama nchi hiyo ya Amerika Kusini, ikiwa bado mamilioni ya fedha zinatumika kila mwaka kuhukumu wahusika pamoja na kutafuta mabaki ya maelfu ya watu waliouwawa na kutoweka wakati wa tukio hilo.

Obama aliuelezea utawala huo wa kidikteta wa baina ya mwaka 1976 hadi1983 kipindi ambacho wanajeshi wa Argentina waliwauwa zaidi ya watu 30,000 kuwa ni kipindi cha giza katika historia ya nchi hiyo. Lakini kiongozi huyo hakuomba msamaha kwa niaba ya Marekani kwa kuunga mkono mapinduzi hayo.

“Niko hapa Buenos Aires kwa sababu mheshimiwa Rais dunia imegundua namna mlivyo tayari kushirikiana tena na jumuiya ya kimataifa na kuimarisha uongozi wa kimataifa wa Argentina ambao unakumbukwa kihistoria. Na hilo tunalikaribisha sana,” amesema Barack Obama

Marekani kuweka wazi nyaraka za kijeshi

Argentinien Barack Obama tanzt Tango
Rais Barack Obama akicheza Tango ArgentinaPicha: Reuters/C. Barria

Obama pia ameahidi kuziweka wazi nyaraka za jeshi la Marekani na idara zake za ujasusi zinazohusika na wakati wa utawala huo wa kidikteta, kipindi ambacho Marekani iliunga mkono serikali kadhaa za Amerika Kusini zilizokuwa zikifuata siasa za mrengo wa kulia

Ziara ya Obama nchini humo ni ishara ya kuunga mkono mageuzi ya kisiasa ya rais Mauricio Macri. Rais aliyemtangulia Cristian Fernandez mara nyingi alikuwa akivutana na Marekani na kupelekea nchi hizo kutokuwa na uhusiano mzuri.

Obama amesema anafurahishwa kuiona Argentina inadhamiria kuimarisha haki za binaadamu, lakini wapinzani wa Marci wanamtilia shaka kuwa kiongozi huyo mhafidhina wa siasa za kisoshalisti anaweza kuwa mtetezi wa haki za binaadamu.

Rais Obama aliwasili Argentina akiwa anatokea nchini Cuba, ambapo alijadiliana na rais wa nchi hiyo Raul Castro masuala ya haki za binaadamu pamoja na uhuru wa kisiasa, wakiwa wanajaribu kumaliza uhasama ulikuwepo baina ya nchi hizo mbili kwa miongo kadhaa ulioanza mara tu baada ya mapinduzi ya Cuba ya mwaka 1959.

Obama anatarajiwa kurejea Marekani jioni leo, akikamilisha ziara yake iliyokuwa na lengo la kuimarisha mahusiano na nchi za ukanda wa Amerika Kusini licha ya kuwepo kwa mahusiano yasiyo mazuri kwa muda mrefu.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ape

Mhariri: Yusuf Saumu