Obama kukutana na Netanyahu na Abbas
21 Septemba 2009Rais Barack Obama wa Marekani ana matumaini ya kuzifufua harakati zinazosua sua za amani ya Mashariki ya Kati wakati wa mazungumzo ya pande tatu yanayofanyika wiki hii, yakayowahusisha Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, na kiongozi wa Wapalestina Mahmud Abbas.
Ikulu ya Marekani ilisema rais Obama atakutana na viongozi hao wawili leo kwa nyakati tofauti, pembezoni mwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa, kabla ya kufanya mkutano wa pamoja na viongozi hao wawili mahasimu.
Katika taarifa yake msemaji wa Ikulu ya Marekani Robert Gibbs, amesema Mazungumzo hayo yatalenga zaidi kuweka msingi wa kuanzisha majadiliano mengine, na kubuni mkutadha mwafaka ili majadiliano hayo yaweze kufanikiwa.
Wizara ya Ulinzi ya Israel ilisema bila kutoa ufafanuzi zaidi kuwa, kabla ya mkutano huo, Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak jana alikutana na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates.
Mazungumzo hayo ya pande tatu ni ya kwanza kufanyika kati ya viongozi hao, tangu rais Obama alivyoingia katika Ikulu ya White House mwezi Januari, akishadidia kuwa ufumbuzi wa amani Mashariki ya Kati ni suala linalopewa kipaumbele na utawala mpya wa chama chake cha Democratic.
Mazungumzo hayo yanakuja punde tu baada ya mjumbe wa Marekani katika Mashariki ya Kati George Mitchel, kurejea mikono mitupu kutoka katika mpango ulioshindwa wa kuwashawishi viongozi wa Israel waache ujenzi wa makazi ya walowezi.
Afisa mmoja wa Ikulu ya Marekani ameonya juu ya matarajio ya kufikiwa makubaliano.
Afisa huyo amesema Obama ambaye alikutana kwa nyakati tofauti na Netanyahu na Abbas katika Ikulu ya Marekani mwezi Mei, anaamini kuwa ni muhimu kwa viongozi hao kukutana wote katika chumba kimoja, na kuendelea kujaribu kuunganisha nyufa.
Afisa huyo ambaye hakutaka kujulikana, pia alipinga kuwa ni muhimu mkutano huo wa pande tatu, unafanyika mapema sana baada ya uvamizi wa Israel ulioacha madhara makubwa dhidi ya ukanda wa gaza mwezi Disemba mwaka jana, na uundwaji wa serikali mpya ya Israel.
Benjamini Netanyahu mwenyewe akizungumzia juu ya mkutano huo, alisema"Sijui. Sina hata fikra. mkutano huo haujawekwa wazi, lakini nadhani utafanyika. Sikuomba ufanyike, wala sikutoa masharti ya kuitisha mkutano huo."
Afisa mmoja wa Mamlaka ya Palestina ameliambia Shirika la habari la AFP kwamba, mkutano huo wa pande tatu hautakuwa kigezo cha kuanzishwa kwa mazungumzo ya amani na Israel, bali utakuwa ni mkutano wa kawaida tu, kwa sababu mamlaka ya Palestina haipendi kuivunja moyo Marekani ambayo imetaka kufanyika kwa mkutano huo.
Ameongeza kuwa, kuanza kwa mazungumzo ya amani kunategemea zaidi kuachwa kwa ujenzi wa makazi ya walowezi unaofanywa na taifa hilo la kiyahudi katika ukingo wa magharibi.
Naye Mitchel aliyesaidia upatikanaji wa amani katika jimbo lililoharibiwa vibaya na vita la Ireland ya Kaskazini mnamo miaka ya 90, amesema mazungumzo ya leo, ni ishara ya wajibu wa dhati wa Obama, kusaidia kupatikana amani ya Mashariki ya kati.
Mwandishi : Lazaro Matalange/AFPE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman