1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama kukutana na Abbas

9 Juni 2010

Rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kukumbana na shinikizo katika jitihada za kuutanzua mzoz waMashariki ya kati wakati akitarajiwa kukutana na kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas.

https://p.dw.com/p/NmDv
Rais Barack ObamaPicha: AP

Mazungumzo baina ya Rais Obama na Kiongozi wa Wapalestina, Mahmoud Abbas, yanatarajiwa kujikita zaidi katika suala la usalama wa Mashariki ya Kati, kufuatia shambulio jingine lililofanywa na Israel la kuwaua makomandoo wanne wa kipalestina katika mwambao huo.

Msemaji wa kiongozi wa Palestina, Nabil Abu Rdainah, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa Mahmoud Abbas anatarajiwa kumshawishi Rais Obama kuishinikiza Israel kuondoa vizuizi katika ukanda huo ambavyo amevielezea kuwa vimekuwa chanzo cha machafuko katika ukanda huo.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, licha ya kutokuwepo matumaini makubwa ya Israel kukubali kufungua vizuizi hivyo, lakini ameeleza kuwa mazungumzo baina ya viongozi hao yatajikita zaidi katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wa Gaza ambapo Marekani imeonyesha nia ya kutoa misaada, na kujadili mipango ya kuwakwamua kiuchumi wakaazi wa ukanda huo.

Hata hivyo, taarifa za ndani hazikufafanuliwa ni aina gani ya misaada ambayo Marekani itatoa kwa Wapalestina huko Gaza, bila kuingia katika mikono ya kundi la kiislamu la Hamas ambalo linaudhibiti ukanda huo ambapo Marekani linalitaja kuwa katika orodha ya makundi ya kigaidi. Chama cha Hamas kilikishinda chama cha Fatah cha Rais Abbas katika uchaguzi mkuu.

Marekani imekuwa ikitoa misaada mara kadhaa kwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambao unadhibitiwa na chama cha Fatah cha Rais Mahmoud Abbas,ambapo Washington katika mkutano wa wafadhili mwaka 2009 iliahidi kutoa misaada inayofikia dola milioni 900 kwa Wapalestina. Utawala wa Rais Obama umeeleza kuwa mazungumzo baina ya viongozi hao yatajikita zaidi katika kuangalia mustakbali wa mgogoro wa mashariki ya kati.

Mkutano baina ya Rais Obama na Abbas huko Washington unafanyika ikiwa ni wiki moja tu baada ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kukatisha ghafla ziara yake nchini humo kufuatia shambulio la wanajeshi wa Israel kuuvamia msafara wa meli za misaada na kuwaua wanaharakati 9 katika meli hizo.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kwamba Obama anakabiliwa na wakati mgumu zaidi kufuatia kukaribia kwa uchaguzi wa kati huko Marekani mwezi Novemba, ambapo Rais huyo anapaswa kuwa makini, kwa vile Israel bado inakubalika kwa wapiga kura wake na wabunge wa nchi hiyo.

Mahamoud Abbas amekuwa akishikilia msimamo wa Umoja wa mataifa kutaka kuundwe tume huru kuchunguza shambulio la Israel kwa wanaharakati wa msafara wa meli za misaada, kinyume na Marekani ambayo inaunga mkono msimamo wa Israel kutaka kufanya uchunguzi wa ndani usiohusisha jumuiya ya kimataifa.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/ RTRE

Mhariri: Miraji Othman