1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama kujifaragua katika hotuba yake ya mwisho kwa taifa

12 Januari 2016

Ni mojawapo ya nafasi za mwisho za kiongozi huyo zilizobakia kuvutia hisia za mamilioni ya wamarekani kabla ya kumezwa na sauti ya atakayemrithi nafasi yake.

https://p.dw.com/p/1Hc4A
Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: Reuters

Rais Barack obama wa marekani atatoa hotuba yake ya mwisho kwa taifa mbele ya bunge la nchi hiyo, hotuba ambayo inalenga kuvutia uungaji mkono wa juhudi kadhaa alizoaanzisha ikiwemo mkataba wa kibiashara wa nchi za pasifik,kupatikana sheria kali za kudhibiti matumizi na umiliki wa bunduki pamoja na kufungwa kwa gereza la Marekani la Guantamano lililoko nchini Cuba.

Hotuba ya rais Obama aliyopangiwa kuitoa muda usiokuwa mrefu kutoka sasa katika bunge la Marekani ni mojawapo ya nafasi za mwisho za kiongozi huyo zilizobakia kuvutia hisisa za mamilioni ya wamarekani kabla ya kumezwa na sauti ya atakayemrithi nafasi yake. Hotuba hiyo ya Obama inatazamiwa kugubikwa zaidi na masuala ya kisiasa akitegemewa kujikita zaidi katika mambo ambayo anawaachia wamarekani kama urithi baada ya kipindi chake kumalizika.

Aidha rais huyo wa Marekani anatazamiwa kuweka wazi kuhusu mapendekezo ya sheria kadhaa mpya ambazo wenzake katika chama chake cha demokrat wameyaweka katika agenda ya kamepini ya uchaguzi wa rais .Wasaidizi wa rais huyo wanasema atatoa mtazamo wenye kuonesha zaidi matumaini katika msimamo wa Marekani ikilinganishwa na tahmini ya mambo ambayo yamekuwa yakipigiwa upatu na wagombea wa chama cha Replican.

Tayari msemaji wa ikulu ya Marekani Josh Earnest alitoa kauli jumatatu inayolaumu kuwepo kwa mitizamo yenye kutoa ishara mbaya kutoka kwa wagombea urais wa chama cha Republican na hasa kutokana na kura za maoni kuonesha wamarekani wengi wanaiona nchi yake ikielekea kwenye mkondo mbaya.

Bunge la Marekani likisikiliza hotuba ya Obama kwa taifa mwaka 2014
Bunge la Marekani likisikiliza hotuba ya Obama kwa taifa mwaka 2014Picha: Reuters

Kutoka na hilo msemaji huyo wa Ikulu amebaini kwamba rais Obama anaiangalia hotuba yake ya leo kama nafasi muhimu ya kuzungumza na taifa kinagaubaga kuhusu changamoto zinazowakabili kama taifa pamoja na nafasi zilizopo kulikabili hilo.

Miongoni mwa masuala muhimu ambayo yatagusiwa kwenye hotuba hiyo ni pamoja na uwezekano wa kuuyasifia makubaliano ya Nuklia na Iran sambamba na kuimarishwa kwa uhusiano kati ya nchi hiyo ya Marekani na Cuba masuala ambayo yameonekana kama ni mafanikio makubwa kwa taifa hilo lenye nguvu duniani. Halikadhalika inatarajiwa Obama atalitia shime bunge la Marekani kuunga mkono mageuzi ya sheria zinazohusu makosa ya uhalifu.

Pamoja na hilo uwezekano upo wa kugusiwa hatua ya Marekani ya kupambana dhidi ya kundi la dola la kiislamu suala ambalo limezua kauli za kukosolewa serikali na upande wa chama cha Republican.Mbali na yote ikulu ya Marekani inataka kuionesha hotuba ya Obama kama ndio kilelezo cha agenda muhimu za kushughulikiwa nchini humo pamoja na suala hilo kutumiwa katika harakati za kamepini ya uchaguzi wa rais yakitiliwa nguvu masuala kadhaa kama vile suala la udhibiti wa bunduki ambalo yumkini litaendelea kuibuka hata baada ya Obama kumaliza muda wake Madarakani.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman