1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congress wanatilia shaka hatua za Obama kwenye kodi

Mohammed Khelef20 Januari 2015

Rais Barack Obama atumia hotuba yake ya kila mwaka kujibu ukosoaji wa Congress linalotawaliwa na Republican juu ya msimamo wake wa kupandisha kodi kwa matajri ili kulisaidia tabaka la kati.

https://p.dw.com/p/1ENJl
Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: picture-alliance/AP Photo/Carolyn Kaster

Akiangazia zaidi kwenye kujijengea jina zuri ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyobakia madarakani, Obama atajitokeza mbele ya kikao cha pamoja cha baraza la Congresss katika majengo ya Ikulu na hotuba yake hapana shaka itawavutia mamilioni ya raia wa Marekani kuifuatilia kupitia televisheni zao.

Kubwa kuliko yote kwenye hotuba hiyo, Obama atashinikiza ongezeko la kodi kufikia dola bilioni 320 ndani ya kipindi cha miaka kumi kwa matajiri, kodi ambayo itakusanywa kwa kuziba mianya na kuzitoza malipo makubwa kampuni zinazojihusisha na masuala ya fedha. Fedha hizo baadaye ndizo zitakazotumiwa kuliinua tabaka la kati kwa kuongeza mapato yao.

Katika vidio iliyotumwa mtandaoni na Ikulu ya Marekani ikiitangazia hotuba hiyo ya leo, Obama anasema atatumia fursa hiyo kuonesha muelekeo wa kuivusha Marekani baada ya miaka sita ya kupambana na mkwamo wa kiuchumi.

"Hotuba hii kwa taifa inanipa nafasi ya kuwafafanulia Wamarekani kwamba vipi baada ya kutoka kwenye mzozo wa kifedha tunaweza sasa kuhakikisha kuwa kila mtu kwenye nchi hii anachangia kwenye ukuwaji wa uchumi na vipi kila mtu anakuwa na nyenzo za kumuwezesha afanikiwe," anasema Obama kwenye vidio hiyo.

Kodi kubwa kwa matajiri

Obama anasema dhamira ya hatua yake hiyo ni kuwasaidia wale walioachwa nyuma na kipindi cha miaka sita ya utawala wake wakati Marekani ikijifufua upya kiuchumi, kilichoanza na serikali ya Democrat anayoiongoza kukabiliana na mserereko wa kifedha.

Rais Barack Obama akizungumza na Spika wa Bunge, John Boehner.
Rais Barack Obama akizungumza na Spika wa Bunge, John Boehner.Picha: Getty Images/Afp/Jim Watson

Obama anasema Wamarekani waliokwishaumia sana kwa machungu ya kuporomoka kwa uchumi, wanastahiki kutunzwa, na kwamba lazima baraza la Congress liuone ukweli huo. "Kwa kipindi cha miaka sita tumeumizwa na nguvu za mporomoko wa kifedha, na kwa sababu ya uvumilivu mkubwa wa watu wa Marekani, nchi hii sasa ina fursa ya kubadilisha hali ya mambo, lakini msingi wa hayo ni kufanya uamuzi sahihi."

Tayari mapendekezo ya Obama yameanza kutiliwa shaka na wajumbe wa chama cha Republican ambao ndio wanaolidhibiti baraza la Congress na ambao hawana nia yoyote ya kupandisha kodi kwa mtu yeyote.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga