Obama kuhutubia taifa kuhusu deni la Marekani
15 Julai 2011Baada ya siku kadhaa za mjadala mkali na onyo la kushushiwa viwango vya uwezo wa kulipa deni, Rais Obama amewaambia wabunge kwamba sasa umewadia wa kufanya maamuzi, na kwamba anataka wafikiane makubaliano haraka ili "wasonge mbele".
Makampuni ya viwango ya Moody's na Standard and Poor's, yameionya Marekani inaweza kupoteza nafasi yake ya kuwa mlipaji mkubwa wa madeni yake. Mkopeshaji mkubwa wa Marekani, China, soko la hisa la Wall Street na Hazina ya Taifa, wote wameonesha shaka zao.
Rais Obama ameondoa kabisa uwezekano wa kukubaliana na utatuzi wa muda mfupi, ili kuyaruhusu majadiliano yaendelee zaidi ya Agosti 2, ambapo Ikulu ya Marekani itakuwa imekosa fedha za kulipia hata huduma muhimu.
Waziri wa Fedha wa Marekani, Tim Geithner, ameonya kwamba kama wabunge wa Republican na Democrat hawakufikia makubaliano ya kuinusuru hali, basi Marekani itakabiliwa na wakati mgumu sana.
"Wakati unatuishia. Macho ya nchi yako kwetu, na macho ya dunia yako kwetu. Tunapaswa kuhakikisha kuwa tusimama pamoja na kupeleka ujumbe wa wazi kwamba tutachukua hatua zinazostahiki kuepuka kushindwa kulipa deni." Amesema Geithner.
Maafisa wa Democrat na Republican wamesema kwamba Rais Obama amewapa viongozi wa vyama vyao bungeni muda wa masaa 24 hadi 36 wawe wameshaafikiana juu ya mswaada wa kupitishwa kwenye Bunge la Congress.
Wachumi, watu wa fedha na wafanyabiashara, wameonya kuwa kushindwa kwa Marekani kupandisha uwezo wake wa kukopa, kunaweza kuutikisa uchumi wa dunia ambao bado haujapona majeraha yake ya mwaka 2008. Kufikia Agosti 2, Marekani inatakiwa iwe imepandisha uwezo wake wa kukopa kutoka kiwango cha sasa cha dola trilioni 14.3.
Hata hivyo, wabunge wa Republican wametaka kuwepo kwa makato ya jumla-jamala wakitafautiana na ombi la Rais Obama la kuongezwa makato kwa matajiri na makampuni makubwa tu.
Spika wa Baraza la Wawakilishi kutokea chama cha Republican, John Boehner, amesema "hakuna chochote ambacho utawala wa Rais Obama unapendekeza kinachoweza kutatua tatizo lililopo". Boehner amemtaka Rais Obama kukata matumizi ya serikali yake kwa kiwango kikubwa.
Naye kiongozi wa wawakilishi wa Democrat, Nancy Pelosi, amesema kwamba wajumbe wa chama chake wanakubaliana na wazo la kukata kiwango fulani cha matumizi kisichozidi dola trilioni 4, lakini hawakubaliani na ukatwaji wa matumizi kwenye sekta ya ustawi wa jamii, kwani huko kutaathiri sana maisha ya watu wa kawaida.
"Hili ni jambo la kibinafsi zaidi, na lenye athari kubwa kwa familia za Wamarekani. Huu ni wakati ambapo meza ya jikoni na meza ya ofisini zina hofu inayofanana." Amesema Pelosi.
Bado haijawa wazi ikiwa Democrat na Republican watakubaliana katika mpango huu wa kuongeza uwezo wa kukopa wa serikali, lakini lililo wazi ni kwamba matokeo yoyote yawayo yataziathiri siasa na uchumi wa Marekani kwa muda mrefu, hasa katika wakati ambapo Rais Obama anajitayarisha kugombea tena uraisi hapo mwakani.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman