1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama kuhimiza vikwazo zaidi dhidi ya Urusi

25 Aprili 2014

Rais Barack Obama wa Marekani Ijumaa (25.04.2014) anatarajiwa kuwashinikiza washirika wake wa Ulaya kuiwekea vikwazo zaidi Urusi iwapo nchi hiyo itazidi kuimarisha vitendo vyake vya uchokozi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/1Bocl
Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: Reuters

Rais Barack Obama wa Marekani amesema atahakikisha kwamba viongozi wakuu wa Ulaya wanakubaliana na maoni yake kwamba Urusi imeshindwa kutimiza masharti ya mkataba wa amani uliofikiwa mjini Geneva mapema mwezi huu ambapo kwayo Urusi,Marekani na Umoja wa Ulaya zilikubaliana kushirikiana kufanikisha usalimishaji wa silaha wa makundi ya watu wenye silaha yalioko kinyume na sheria.

Amesema "Kuna fursa kwa Urusi kuchukuwa msimamo tafauti na tunawashajiisha kufanya hivyo. Wakati huo huo tutajiandaa kuchukuwa hatua zaidi iwapo Urusi itashindwa kuchukuwa msimamo tafauti."

Obama amesema tayari vikwazo vyao vimekuwa na taathira kwa uchumi wa Urusi na hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi lakini hawana utashi wa kuwaumiza wananchi wa kawaida wa Urusi.

Obama ambaye ameishutumu Urusi kwa kuwatuma majasusi kuratibu machafuko mashariki ya Ukraine kama ilivyofanya kabla ya kulinyakua jimbo la Crimea hapo mwezi wa Februari anatazamiwa kuzungumza na washirika wake wa Ulaya baadae leo hii.

Operesheni ya kuwatimuwa waasi

Vikosi vya Ukraine vimeuwa takriban waasi watano wanaoiunga mkono Urusi hapo jana wakati walipokuwa wanaisogelea ngome kuu ya mashariki mwa Ukraine na Urusi imeanzisha mazoezi ya kijeshi karibu na mpaka na Ukraine na kuzusha hofu kwamba vikosi vyake hivyo yumkini vikaivamia nchi hiyo.

Jeshi la ulinzi la Ukraine likiwa nje ya mji wa Slaviansk mashariki ya Ukraine.
Jeshi la ulinzi la Ukraine likiwa nje ya mji wa Slaviansk mashariki ya Ukraine.Picha: picture-alliance/ITAR-TASS

Vikosi maalum vya Ukraine vimeanzisha awamu ya pili ya opereseheni yao ya kijeshi dhidi ya wanaharakati wanaotaka kujitenga mashariki mwa nchi hiyo leo hii kwa kuuzingira kikamilifu mji unaoshikiliwa na waasi wa Slaviansk.

Mojawapo ya helikota zake za kijeshi imepigwa na roketi na kuripuka wakati ikiwa katika kambi ya kijeshi karibu na mji huo.

"Uwenda wazimu unaotokea Ukraine "

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Sreinmeier ameonya leo hii wakati unayoyoma kushughulikia kile alichokiita "uwenda wazimu" unaotokea huko Ukraine ambapo hali ya mvutano inazidi kupamba moto kwa kile serikali ya Ukraine ilichosema ni juhudi za Urusi kuchochea Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier (Kushoto) na mwenzake wa Ufaransa Laurent Fabius (Kulia) wakiwasili Tunis, Tunisia.(24.04.2014)
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier (Kushoto) na mwenzake wa Ufaransa Laurent Fabius (Kulia) wakiwasili Tunis, Tunisia.(24.04.2014)Picha: Fethi Belaid/AFP/Getty Images

Steinmeier yuko ziarani nchini Tunisia na waziri mwenzake wa Ufaransa Laurent Fabius wote wametowa wito wa kuuzima mzozo huo uliozidi kupamba moto baada ya jeshi la Ukraine kuanzisha shambulio kuu la kuwatimuwa waasi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tunis Steinmeier amesema hakuna muda wa kutosha kuukomesha mzozo huo na kuzitaka pande zote ndani ya Ukraine yenyewe na wale wanaouwanga mkono nje ya nchi hiyo kurudisha fahamu zao na kutumia busara.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman