1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama : Igeni mfano wa Mandela

29 Juni 2013

Rais Barack Obama wa Marekani Jumamosi(29.07.2013) amewashajiisha viongozi wa Afrika na duniani kwa jumla kufuata mfano wa rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela kwa kulitanguliza mbele taifa kabla ya nafsi yake.

https://p.dw.com/p/18yXm
Rais Barak Obama ziarani Afrika Kusini.
Rais Barak Obama ziarani Afrika Kusini.Picha: Reuters

Obama amesema wakiwa kama viongozi wanashikilia nyadhifa hizo kwa muda na wasidanganyike kiasi cha kufikiri kwamba hatima ya nchi yao haitegemei kadiri watakavyoendelea kuwa madarakani.

Obama alikuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliomjumuisha pia Rais Jacob Zuma mjini Pretoria akiwa katika ziara yake ya wiki moja barani Afrika ambayo tayari imemfikisha Senegal na anatazamiwa kuzuru Tanzania hapo Jumatatu. Obama anafanya ziara hiyo wakati nchi nyingi za Kiafrika zikiwa kwenye mizozo ya kidini, kikabila na mengineyo.

Sio wakati muafaka kuzuru Kenya

Obama ameamuwa kukwepa kuizuru Kenya kwa sababu ya nchi hiyo kuhusika kwenye mzozo wa kimataifa. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imemfungulia mashtaka Rais Uhuru Kenyatta kwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu yakiwemo mauaji kuhamisha watu kwa nguvu, ubakaji,ukandamizaji na vitendo vya kinyama vilivyofanywa na wafuasi wake kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.Picha: Reuters

Obama amekaririwa akisema "Wakati sio muafaka akiwa kama rais wa Marekani kuitembelea Kenya wakati masuala hayo yakiwa bado yanafanyiwa kazi na nataraji yatapatiwa ufumbuzi." Amesema tayari ametembelea Kenya mara kadhaa na ataitembelea tena nchi hiyo kipindi cha usoni.

Obama na Zuma walikuwako kwenye Majengo ya Umoja ambako ndiko kuliko ofisi za serikali na ndiko mahala ambapo Mandela alikoapishwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini hapo mwaka 1994 baada ya kuwa gerezani kwa miaka 27 kwa harakati zake za kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.

Mandela mwenye umri wa miaka 94 amelazwa katika hospitali mjini Pretoria kwa wiki tatu sasa kutokana na maambukizi ya mapafu. Zuma amewaambia waandishi wa habari hali ya Mandela ni mbaya lakini imara na kwamba taifa zima linamuombea apone.

Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini katika mkutano na waandishi wa habari (29.06.2013).
Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini katika mkutano na waandishi wa habari (29.06.2013).Picha: Reuters

Obama na mke wake wamekutana na baadhi ya ndugu wa familia ya Mandela lakini kutokana na matakwa yao hakupanga kumuona Mandela ambaye ni mmojawapo wa watu adhimu kabisa duniani.

Obama akimtaja Mandela kwa jina lake la kiukoo amepongeza mjumuiko wa kijamii wa Afrika Kusini kutoka utawala wa kibaguzi na kusema kuwa ni alama inayon'gara duniani.

Mandela shajiisho la dunia

Obama amesema mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi kwa ajili ya uhuru,moyo ya uadilifu wa Madiba kipindi cha nchi cha kihistoria cha taifa hilo kubadilika na kuwa huru na la demokrasia yamekuwa ni mambo yaliomshajiisha yeye mwenyewe binafsi na kuwa kichocheo kwa dunia.

Nelson Mandela alama ya mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi.
Nelson Mandela alama ya mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi.Picha: DW

Zuma amemwambia Obama kwamba yeye na Mandela wamefungamanishwa na historia kwa kuwa marais wa kwanza weusi kwa nchi zao na kwa kuwasilisha matumani ya mamilioni ya watu barani na Afrika na wale wanaoishi nje ambao huko nyuma walikuwa wakikandamizwa.

Katika masuala mengine Obama amekataa kujifunga moja kwa moja katika kuunga mkono juhudi za Afrika Kusini kuwania kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.Amesema mfumo wa Umoja wa Mataifa unahitaji kurekebishwa na litakuwa sio jambo la kawaida kulitanuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa bila kujumuisha uwakilishi wa Afrika.

Uwekezaji wa China haumtishi

Obama pia amesema anataka kuimarisha biashara na Afrika na kuanzisha mazungumzo mapya ya mkataba wa biashara na Afrika ili kuuboresha kwa kampuni za biashara za Marekani.Pia amesema anakaribisha juhudi kubwa zinazofanywa na nchi nyengine kutafuta fursa za biashara barani Afrika ikiwemo China.

Rais Barak Obama katika mkutano na waandishi wa habari Pretoria (29.06.2013).
Rais Barak Obama katika mkutano na waandishi wa habari Pretoria (29.06.2013).Picha: Reuters

Amesema hatishwi na jambo hilo na anafikiri ni zuri ila tu ushauri wake ni kuhakikisha tu kwamba ni kwa ajili ya manufaa ya Afrika kwa kuhakikisha miradi ya uwekezaji ya kigeni inawaajiri Waafrika,haindekezi rushwa au kuchukuwa rasimali zake za asili bila ya kuwafidia Waafrika.

Umuhimu wa Soweto

Obama pia ametowa heshima zake kwa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini kwa kutembelea kitongoji cha Soweto ambapo amehutubia wanafunzi katika ukumbi wa jiji wa Chuo Kikuu cha Johannesburg.Takriban vijana 176 wameuwawa katika kitongoji cha Soweto wakati wa maandamano ya vijana dhidi ya marufuku ya utawala wa ubaguzi wa rangi ya kufundisha lugha za kienyeji za Kibantu.Uasi wa Soweto uliimarisha uungaji mkono wa kimataifa dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi na mwezi wa Juni hivi sasa unatambulika kuwa ni Mwezi wa Vijana nchini Afrika Kusini.

Kitongoji cha Soweto.
Kitongoji cha Soweto.Picha: Jana Genth

Obama atakamilisha ziara yake Afrika Kusini Jumapili ambapo anapanga kutowa hotuba kubwa kuhusu sera ya Marekani kwa Afrika katika Chuo Kikuu cha Cape Town na ataipeleka familia yake katika kisiwa cha Robben kuzuru gereza ambalo Mandela alitumikia miaka 18 ya kifungo chake cha miaka 27 gerezani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri : Yusuf Saumu