Obama azungumza na Rouhani kwa njia ya simu
28 Septemba 2013Mahusiano ya kidiplomasia baina ya Marekani na Iran yamepiga hatua moja mbele hapo jana, kufuatia mazungumzo hayo ya simu baina ya Obama na Rouhani. Hayo ndiyo yaliyokuwa mazungumzo ya kwanza kabisa baina ya Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa zaidi ya miongo mitatu iliyopita.
Rais Obama alithibitisha kuwa mawasiliano hayo ya simu yalifanyika wakati alipozungumza na waandishi habari katika Ikulu ya White House baadaye jana Ijumaa. Tukio hilo pia lilithibitishwa kupitia taarifa rasmi iliyochapishwa kwenye tovuti ya ofisi ya rais ya Iran.
Tovuti ya Rais Rouhani imesema “Marais hawa wawili wamesisitiza kuhusu nia ya kisiasa ya kuwepo azimio la haraka kuhusu suala la nyuklia, pamoja na kutoa nafasi ya kutatua masuala mengine na ushirikiano wa masuala ya kikanda”.
Kuendeleza mazungumzo
Obama na Rouhani walijadili kuhusu mipango yao ya kuendelea mbele na mazungumzo haraka iwezekanavyo. Mawasiliano hayo ya simu yalifanywa wakati Rais huyo wa Iran alipokuwa njiani kuelekea katika uwanja wa ndege. Obama amewaambia waandishi wa habari “hata ingawa kutakuwepo na vikwazo vikubwa katika kusonga mbele na kupata mafanikio, naamini kuwa tunaweza kufikia suluhisho kamili”.
Uhusiano baina ya nchi hizo mbili uliharibika mwaka wa 1980, mwaka mmoja baada ya vuguvugu la mageuzi la Iran lilipouangusha utawala uliokuwa ukiunga mkono Marekani, na kuwaweka madarakani viongozi wanaofuata nadharia kali za kiislamu. Vuguvugu hilo pia lilisababisha mzozo uliodumu siku 444 katika ubalozi wa Marekani mjini Tehran ambapo jumla ya Wamarekani 52 walishikiliwa mateka na wanafunzi wenye itikadi kali za kiislamu hadi Januari mwaka wa 1981.
Rais wa Iran alianza kutengeneza mahusiano punde baada ya kuchukua madaraka mwaka huu. Kabla tu ya ziara yake katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York wiki hii, alidokeza nia ya serikali yake kushiriki mazungumzo kuhusu mpango wa kutengeneza nishati ya nyuklia. Amesema Iran haina nia ya kutengeneza bomu la nyuklia na akarudia madai ya awali kuwa serikali yake inataka tu kurutubisha madini ya urani kwa sababu za amani pekee.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Iran, Mohammed Javad Zarif wamepewa jukumu la kufuatilia mkutano wa viongozi wa ngazi ya juu ili kuanza kuweka kazi ya msingi kuhusu ushirikiano zaidi baina ya nchi hizo mbili. Mapema Ijumaa, Rouhani alisema anataka kuyatumia mazungumzo yajayo ya nyuklia kusaidia kuweka imani baina ya Iran na viongozi wa Kimataifa. Aliwaambia waandishi wa habari “mazingira ni tofauti sana kuliko jinsi yalivyokuwa katika siku za nyuma. Lengo letu ni maslahi ya pamoja baina ya mataifa mawili. Lengo letu ni kutatua shida zetu. Lengo letu ni kujenga imani hatua kwa hatua baina ya serikali na viongozi wa kimataifa”.
Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Sekione Kitojo