Mpango wa Obama wa kudhibiti silaha wakosolewa
6 Januari 2016Rais Barrack Obama amezungumza kwa masisitizo wakati alipokuwa akitangaza mpango wake wa kudhibiti silaha na mikakati mengine ambayo imekosolewa na makundi ya kutetea silaha ambayo Rais Obama ameyashutumu kwa kuliteka nyara bunge la Congress.
Kwa masikitiko makubwa huku akiweka mkono wake chini ya kidevu chake rais Obama alijifuta machozi wakati alipokuwa anakumbuka mauaji ya halaiki yaliofanywa mwaka wa 2012 katika shule ya msingi ya Sandy Hook mjini Newtown, Obama alisema anasikitishwa na hatua ndogo zilizopigwa dhidi ya udhibiti wa silaha tangu watoto takriban 20 wa shule ya msingi walipouwawa, nchini humo, tukio lililolishitua taifa zima la Marekani.
Mpango huo wa vipengele 10 wa Rais Obama unajumuisha kupunguza udhibiti wa silaha na upatikanaji wa leseni kwa wauza silaha pamoja na kufanya ukaguzi wa historia ya wanaonunua silaha hizo.
"Namba moja, mtu yeyote aliye katika biashara ya uuzaji silaha lazima apate leseni na afanye ukaguzi wa historia ya wateja au atahukumiwa kwa makosa ya uhalifu, haijalishi iwapo unafanya kazi hiyo kupitia mtandaoni au katika maonyesho ya silaha, haijalishi unafanyia wapi kazi yako lakini kinachokitajika ni kile unachokifanya. Tunaangalia ukaguzi wa wateja ili kudhibiti uhalifu kwa kuwazuwiya wahalifu kuendelea kununua silaha hatari kwa kujificha nyuma ya mashirika kadhaa na maeneo mengine," alisema rais Obama.
Hata hivyo, Obama alisema wazi kuwa hatua hizo alizozipitisha bila ya kulishirikisha bunge la Congress, hazitoweza kumaliza kabisa matumizi mabaya ya silaha.
Wakosoaji waupinga mpango wa Obama wa kudhibiti silaha
Huku hayo yakiarifiwa, wakosoaji wa Rais Obama wamesema mpango huo ni hatua isiyokubalika kwa wamarekani na inayowanyima raia wa nchi hiyo haki yao ya kikatiba, huku wanachama wa Republican wakisema wataupinga mara moja mpango huo iwapo watashinda uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Mgombea wa chama hicho, Jeb Bush, amesema badala ya kuwapokonya silaha Wamarekani wanaoheshimu sheria, jambo linalofanywa na Obama pamoja na mgombea wa chama cha demokrats Hillary Clinton, wangezingatia kuhakikisha silaha haziingii mikononi mwa magaidi wanaotaka kusababisha vifo vya Wamarekani wasiokuwa na hatia.
Aidha Chama cha wamiliki wa silaha cha Marekani NRA, kilikosoa vikali tangazo la Obama huku muakilishi wa chama hicho akisema hatua za Rais Obama zinakiuka madaraka yake na zimelengwa kuwabebesha dhamana wanaomiliki silaha.
Kwa upande mwengine wanachama kadhaa wa Democrat wameuunga mkono mpango wa Obama huku Hilarry Clinton akimshukuru Obama katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter kwa kusema "Ahsante kwa kuchukua hatua muhimu za kudhibiti silaha, rais anayefuata anapaswa kuendeleza mpango huo na sio kuuondoa."
Mwandishi Amina Abubakar/AP/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef