1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama awasilisha mpango wa kuifunga Guantanamo

24 Februari 2016

Rais wa Marekani Barack Obama amezindua mpango wa mwisho jana (23.02.2016) wa kulifunga gereza la Guantanamo Bay nchini Cuba, akitumai kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni kabla kuondoka madarakani Januari 2017.

https://p.dw.com/p/1I0sU
Kuba US-Gefangenlager Guantanamo Bay
Picha: picture-alliance/dpa/US Navy/Shane T. McCoy

Akiwa amebakisha chini ya mwaka mmoja katika awamu yake ya mwisho madarakani, rais Obama aliwasilisha mpango wa kulifunga gereza la Guantanamo, akilieleza kama doa kwa sifa na hadhi ya Marekani na kichocheo kwa magaidi.

"Sitaki kulikabidhi tatizo hilo kwa rais anayekuja, yeyote yule, na ikiwa kama taifa hatutalishughulikia suala hili sasa, tutalishughulikia lini? Je tutaliacha kwa miaka mingine 15, 20 au 30? Kama hatutafanya tunachotakiwa, nadhani vizazi vijavyo vitaangalia nyuma na kuuliza kwa nini tulishindwa kuchukua hatua wakati sababu sahihi, upande sahihi wa historia na tamaduni nzuri kabisa za Marekani ulikuwa wazi."

Obama aliainisha mpango utakaogharimu kati ya dola milioni 290-475 za kimarekani kuwahamisha wafungwa 91 waliobakia katika gereza hilo kuwapeleka katika nchi za kigeni na katika jela moja kati ya 13 za Marekani ambazo hazikutajwa.

Obama alisema gereza la Guantanamo linaathiri vita dhidi ya ugaidi kwa sababu magaidi wanalitumia kama propaganda katika juhudi zao za kuwasajili wafuasi. Pia alisema gereza hilo linatumia fedha nyingi katika bajeti ya jeshi, huku karibu dola milioni 450 zikitumika mwaka uliopita pekee kuliendesha, na dola milioni 200 kama gharama za ziada kwa washukiwa chini ya 100.

USA Barack Obama Plan zur Schließung Guantanamo Bay
Rais Barack Obama, katikati, makamu wa rais Joe Biden, kushoto, na waziri wa ulinzi, Ashton Carter, kuliaPicha: picture-alliance/dpa/S. Thew

"Kuendelea kukiweka wazi kituo hiki ni kinyume na maadili yetu. Inaharibu hadhi yetu ulimwenguni; kinaonekana kama doa katika rekodi yetu jumla ya kuwa na viwango vya juu kabisa vya utawala wa sheria."

Kwa sasa kuna wafungwa 91 waliobakia Guantanamo, 35 kati yao wakiwa tayari wamechunguzwa na kuidhinishwa waachiwe huru. Washukiwa 800 walizuiliwa katika gereza hilo wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush.

Katika mpango wa rais Obama, bodi maalumu za wachunguzi zitatathmini ni wafungwa gani kati ya 56 waliosalia ambao wanastahili kuachiwa na kupelekwa katika mataifa mengine. Wale ambao hawataidhinishwa watazuiliwa katika jela moja nchini Marekani.

Umoja wa Mataifa uliupongeza mpango wa kuifunga jela la Guantanamo. Stephane Dujarric, msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, alisema, "Ofisi ya Haki za binaadamu inarudia tena wato wake kwamba wafungwa wote waachiwe na wapelekwe nchini kwao au katika nchi ya tatu, iwapo watakuwa katika hatari ya kuteswa ama wahamishiwe katika jela ya kawaida ya Marekani au nchi nyingine kesi zao zikasikilizwe kwa haki kuingana na sheria za kimataifa."

Upinzani wajitokeza dhidi ya mpango wa Obama

Spika wa bunge la Marekani Paul Ryan alilikataa pendekezo la Obama akisema kuwaleta magaidi wa Guantanamo Marekani si jambo la busara wala salama. "Ni kinyume na sheria, na itabaki kuwa kinyume na sheria," akaongeza kusema Ryan.

Kabla wafungwa kuhamishiwa Marekani ikulu italazimika kutambua kituo ambako wanaweza kuzuiwa. Jela 13 zimeshatambuliwa na wizara ya ulinzi, Pentagon. Hata hivyo bunge limemuwekea vikwazo rais Obama.

Guantanamo Gefangenlager Wachmann Zelle Gefangene
Mwanajeshi wa Marekani akilinda jela ya Guantanamo, huku wafungwa wakiangalia majarida na vitabu Machi 30, 2010Picha: picture-alliance/Everett Collection/J. Nistas

"Kwa kuwa bunge limeweka sheria zinazozuia kuwahamishia wafungwa nchini Marekani, hii itakuwa changamoto na tuendelea kulihimiza bunge kwamba tunaweza kuwaleta kwa njia ya kuwajibika na salama, kuzingatia tuliyojifunza na rekodi madhubuti ya jela zetu zenye ulinzi mkali," alisema Obama.

Kulishawishi bunge kuondoa vikwazo vya kisheria kitakuwa kibarua kipevu kwa Obama. Hata wakati chama cha Democratic kilipokuwa na idadi kubwa ya wabunge 2010, bunge lilikataa kuidhisha fedha za kuwahamisha wafungwa wa Guantanamo hadi Marekani. Sasa chama cha Republican kinalidhibiti bunge na baraza la seneti.

Na huu ukiwa ni mwaka wa uchaguzi Marekani, wagombea watatu wa chama hicho wanaoongoza - Donald Trump, Ted Cruz na Marco Rubio, wote wanapinga hatua ya kulifunga gereza la Guantanamo.

Kwa mujibu wa utafiti wa maoni uliofanywa na tasisi ya Rasmussen, asilimia 53 ya Wamarekani wanapinga kufungwa gereza hilo huku asilimia 29 wakiunga mkono.

Obama amejaribu kulifunga gereza la Guantanamo kwa karibu miaka minane, lakini amekwamishwa na bunge, wizara yake ya ulinzi na baadhi ya viongozi katika chama chake cha Democratic, pamoja na washirika wa kigeni wanaokataa kuwachukua washukiwa wa ugaidi.

Mwandishi:Kimball, Spencer (Chicago)

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Grace Kabogo