1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa zapamba moto kuelekea uchaguzi Marekani

12 Oktoba 2016

Obama amewakanya Warepublican kwa kuwa upande wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais licha ya kumkosoa kuhusu vidio iliyomuonyesha akijinasibu kuwa na uwezo wa kuwadhalilisha wanawake kijinsia. 

https://p.dw.com/p/2R945
US-Präsident Barack Obama macht eine Aussage über das Pariser Abkommen
Rais Barack ObamaPicha: Getty Images/AFP/J. Watson

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika North Carolina Rais Obama alisema huwezi kuendelea kukosoa kile kilichosemwa na mtu lakini bado ukaendelea kumuuunga mkono na kuahidi kuwa utamchagua kuwa mmoja wa watu wenye madaraka makubwa duniani.

Akisisitiza juu ya hilo Rais Obama alisema: ''Trump amekuwa akisema mambo mabaya kwa muda sasa, hivi mlifikiria nini, mlidhani kuwa atabadilika, mie mwenyewe kwa sasa na umri wa miaka 55 naona ni vigumu kwangu kubadilika, najua katika umri wa miaka 70 itakuwa ni vigumu zaidi."

Katika mkanda wa vidio hiyo ya mwaka 2005 uliyofichuliwa kupitia vyombo vya habari Ijumaa iliyopita  mgombea huyo wa chama cha Republican alitoa matamshi yanayowadhalilisha wanawake kijinsia ingawa tayari ameshaomba radhi kuhusiana na matamshi hayo.

Kufichuliwa kwa kashfa hiyo kupitia mkanda huo wa vidio kumezidi kuongeza mpasuko ndani ya chama cha Republican ikiwa zimebaki wiki chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini humo, wanasiasa wengi waandamizi ndani ya chama hicho wameanza kujitenga na bilionea huyo.

Rais Obama alisema sio lazima uwe mume au mzazi kukemea kauli kama hiyo iliyotolewa na Donald Trump bali mtu yeyote muungwana hawezi kukubaliana na kauli hiyo na kuwataka Wamarekani kumchagua mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton.

US TV Debatte Trump vs Clinton
Donald Trump akilumbana katika mdahalo wa TV na Hillary ClintonPicha: picture alliance/AP Photo/J. Locher

Ama kwa upande mwingine  mgombea huyo wa chama cha Republican Donald Trump kupitia katika mtandao wa tweeter alionyesha kuwashambulia baadhi ya wanasiasa ndani ya chama cha Republican ambao wanaonekana kutomuunga mkono hali inayoashiria kuzidisha mpasuko mkubwa na kutishia juu ya msitakabali wa baadaye wa chama hicho kikongwe cha kisiasa.

Akionyesha kutobanwa na mifumo ndani ya chama hicho Trump aliwaponda viongozi wa chama cha Republican  kwa kitendo chao cha kutomuunga mkono katika kampeni zinazoendelea na kuahidi kuendelea kupambana  kufanya kampeni zake dhidi ya Hillary Clinton katika siku zilizosalia  kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Donald Trump alimuita mwanasiasa wa ngazi ya juu kutoka katika chama cha Republican ambaye pia ni spika wa bunge la wawakilishi Paul Ryan kuwa ni dhaifu na kiongozi asiye imara.

Aidha Trump alijigamba akisema: "Ni vyema kuwa nimeondokana na minyororo na sasa naweza kuipigania Marekani jinsi ninavyotaka."

Matumaini ya warepublican waliodhania kuwa mgombea huyo ambaye alipata umaarufu kupitia katika vipindi vya televisheni alivyowahi kuviongoza angeweza kushika madaraka hayo kama ilivyokuwa kwa Ronald Reagan lakini matumaini hayo yameonekana kufifia kwa haraka zaidi hasa baada ya kufichuliwa kwa vidio hiyo iliyomuonyesha Trump akitoa matamshi ya kuwadhalilisha wanawake.

Mwandishi: Isaac Gamba/ DPAE/AFPE

Mhariri: Yusra Buwayhid