Obama awaonya walevi wa madaraka Afrika
28 Julai 2015Obama alisema dunia inapaswa kubadili namna inavyolishughulikia bara la Afrika kwa kufanya biashara ya haki badala ya kulipatia tu misaada, na kuahidi ushirikiano wa Marekani katika kupambana dhidi ya magaidi na kukomesha migogoro.
Katika hotuba ya kwanza kabisaa ya rais wa Marekani alieko madarakani kwa Umoja wa Afrika, Obama amesema vurugu zilizosababishwa na azma ya rais wa Burundi kung'ang'ania madarakani zimeonyesha hatari ya kupuuza miongozo ya kikatiba.
"Afrika inasonga mbele, na Afrika mpya inainukia," alisema katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, akiongeza kuwa ukuaji wa kasi wa kiuchumi wa Afrika ulikuwa unabadili dhana za kizamani kwamba Afrika ni bara la vita na umaskini.
Changamoto za ajira kwa vijana
Lakini alisema kuna jukumu la haraka linalolikabili bara hilo ambalo wakaazi wake bilioni moja wataongezeka maradufu katika miongo michache ijayo. "Afrika itahitaji itahitaji kuunda mamilioni ya ajira kuliko inavoyfanya hivi sasa," alisema.
"Tunahitaji tu kuangalia upande wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kuona kwamba idadi kubwa ya vijana wasio na ajira na sauti zilizokandamizwa vinaweza kuchochea ukosefu wa utulivu na machafuko."
Obama alisema viongozi wanapaswa kuheshimu sheria na Umoja wa Afrika laazima uwatie kishindo kutokiuka ukomo wa mihula. "Sijui kwa nini watu wanataka kusalia madarakani kwa muda mrefu, hasa wanapopata pesa nyingi," alisema Obama na kusababisha vicheko kutoka kwenye hadhira ya bara linalojulikana kwa siasa za "mabwana mkubwa" wanaotuhumiwa kwa kufuja fedha za umma.
Akibainisha kuwa alikuwa katika muhula wake wa pili na hangeweza kuhudumu tena, hata wakati akiamini angeweza kushinda tena uchaguzi, Obama alisema: " Natazamia kuwa na maisha baada ya kuwa rais."
Hotuba ya Obama ilihitimisha ziara ya Kenya, taifa alikozaliwa baba yake, na Ethiopia, nchi ambayo kwa wakati fulani ilikumbwa na baa la njaa, ambalo kwa sasa liko njiani kupata ukuaji wa asilimia 10 mwaka huu.
Wakati wa ziara yake yote, Obama alizungumzia ushirikiano wa kiusalama na mataifa yanayopambana dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu nchini Somalia, ukuzaji wa demokrasia na biashara katika bara ambalo tangu mwaka 2009 limefanya biashara kubwa zaidi na China kuliko Marekani.
Katika kile kilichoonekana kama kuipiga madongo China, bila kutaja nchi yoyote, alisema Marekani inatoa ushirikiano ambao hauhusu tu ujenzi wa miundombinu ya mataifa kwa kutumia wafanyakazi wa kigeni au kunyonya rasilimali za Afrika.
China imejenga miundombinu mingi barani Afrika, ikiwemo ya usafiri wa treni za mjini katika jiji la Addis Ababa. Lakini Waafrika wanazidi kuyatuhumu makapuni ya Kichina kwa kutumia wafanyakazi wa kigeni na kuchukuwa bidhaa bila kuongeza thamani yoyote. China inasisitiza yenyewe ni mshirika wa maendeleo.
Akiwa nchini Ethiopia, Obama alifanya mazungumzo na viongozi wa kanda kuhusu mgogoro wa nchini Sudan Kusini. Rais huyo wa Marekani alitoa wito wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya taifa hilo changa kabisaa duniani ikiwa pande zake zinazohasimiana hazitafikia makubaliano ya amani ifikapo Agosti 17.
Alirejelea kitisho hicho katika hotuba yake, wakati akiwatolea mwito viongozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, taifa jengine linalokabiliana na mgogoro, kuheshimu uchaguzi baadaye mwaka huu.
Mapambano dhidi ya ugaidi
Alisema Marekani inasimama bega kwa bega na Afrika ili kuushinda ugaidi na kukomesha migogoro, akionya kuwa maendeleo ya bara hilo yatategemea usalama na amani.
Alibainisha baadhi ya vitisho vinavyoikabili Afrika, vikiwemo kutoka makundi ya Al-Shabaab nchini Somalia, Boko Haram nchini Nigeria, waasi nchini Mali na Tunisia, na kundi la LRA la nchini Uganda.
Obama alisema Marekani inaunga mkono juhudi za Umoja wa Afrika na kuwasifu kama mashujaa, walinda amani wa Afrika wanaopambana dhidi ya wanamgambo.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre
Mhariri: Daniel Gakuba