Obama awafundisha washirika wa NATO Ulaya
4 Juni 2014Mhariri wa gazeti la Badische Neueste Nachrichten anasema kwamba licha ya onyo la Obama kwamba mataifa washirika wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO sasa wachote fedha kutoka makasha ya hazina zao kuimarisha ulinzi, angalau hakuwaacha wakavu. Ameahidi misaada tele ya kijeshi, kifedha na kibinaadamu.
Obama anajaribu kufanya kile kile ambacho Rais Vladimir Putin wa Urusi alikikisia, ikiwa angeliipandisha mori NATO: boti za doria kwenye Bahari Nyeusi, kuwekwa ndege za kivita katika eneo la Baltiki na mazoezi ya kijeshi.
Mhariri wa Stuttgarter Zeitung anazungumzia hilo hilo la Obama na ziara yake ya siku nne barani Ulaya, lakini kwa kuangazia mazungumzo ya hapo jana kwa njia ya simu kati ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Putin wa Urusi.
Mazungumzo haya yanaashiria jaribio la mataifa ya Magharibi kuona ikiwa mkakati wake wenye pande mbili dhidi ya Urusi unaweza kufaa: upande mmoja wa mkakati huo ni kuitisha Urusi na mwengine kuonesha utayari wa kujadiliana nayo. Merkel anajitokeza kama mpenda majadiliano, Obama kama mpenda vitisho.
Ujumbe wa Obama nchini Poland jana ni kwamba uchokozi wa kijeshi wa Urusi hautaweza kukomeshwa kwa mazungumzo pekee, bali kwa hatua kali zaidi za kiuchumi zinazoweza kuiathiri zaidi serikali mjini Moscow kuliko maonyesho ya nguvu za kijeshi.
Kitisho dhidi ya usalama wa ndani
Mhariri wa gazeti la Leipziger Volkszeitung anagusia hofu iliyotajwa na Mwenyekiti wa Vyama vya Wafanyakazi wa Idara ya Polisi hapa Ujerumani, kwamba kuongezeka kwa kuzorota kwa usalama wa ndani kunaweza kupelekea wananchi kuikasirikia serikali yao.
Oliver Malchow amesema wakati akiwasilisha takwimu za uhalifu kwa mwaka 2013 hivi leo, kwamba uhalifu dhidi ya mali umeongezeka, kwa maana ya wizi na uharibifu wa mali za watu. Na hivyo, wananchi ambao wanajiona hawalindwi ni rahisi sasa kukosa imani na mfumo wa ulinzi na hata kuigeuka serikali.
"Sijui", anahoji Malchow, “ni vipi mlipa kodi ambaye sehemu kubwa ya pato lake hwenda kwenye makasha ya serikali, atabakia kimya ikiwa anaamini serikali hiyo haiwezi kumlinda yeye na nyumba, gari au mali yake yoyote?"
Wageni bado wanabaguliwa
Naye mhariri wa gazeti la Rheinische Post anazungumzia takwimu zilizotolewa jana na Kamishna wa Uhamiaji katika Serikali Kuu ya Shirikisho, Aydan Özoguz, juu ya kuendelea kuwepo kwa ubaguzi dhidi ya wageni nchini Ujerumani, licha ya ukweli kuwa raia mmoja katika kila watano ana asili ya kigeni.
"Bado kuna malalamiko ya wazi kwa watuma maombi ya kazi au masomo kwamba majina yenye lafudhi za kigeni yanawekwa kando." Anasema Özoguz, ambaye mwenyewe ni Mjerumani mwenye asili ya Kituruki, akiongeza kwamba sasa Ujerumani ni moja ya nchi zenye wahamiaji wengi zaidi duniani, na hivyo kampuni zinaweza kutumia fursa hiyo kuajiri wafanyakazi wenye ujuzi wa kila aina kutoka mataifa mengine, badala ya kuwachuja.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Vyanzo: Badische Neueste Nachrichten, Rheinische Post, Stuttgarter Zeitung, Leipziger Volkszeitung
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman