1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atetea ufanisi wa uongozi wake wa miaka minane

Oumilkheir Hamidou
5 Januari 2017

Rais wa Marekani, Barack Obama amewatumia risala Wamarekani akitetea mambo muhimu yaliyotekelezwa wakati wa utawala wake wa mihula miwili na hasa kuhusu bima ya afya ambayo rais mteule Donald Trump anadhamiria kuivunja.

https://p.dw.com/p/2VLet
Washington Präsident Obama im Weißen Haus
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. M. Monsivais

Ikulu ya Marekani imechapisha risala hiyo pamoja na ripoti kutoka kila wizara ya Marekani inayozungumzia mafanikio yaliyopatikana tangu Barack Obama alipokabidhiwa hatamu za uongozi wa Marekani miaka minane iliyopita wakati ambapo dola hilo kuu kiuchumi lilikuwa linakurubia kufilisika.

"Katika wakati ambapo nnajiandaa kukabidhi hatamu za uongozi na kutekeleza jukumu langu kama raia wa kawaida, nina fakhari ya kusema tumefanikiwa kujenga misingi imara kwa ajili ya nchi yetu-Marekani", ameandika rais wa 44 wa Marekani katika risala yake.

Miongoni mwa mafanikio muhimu yaliyopatikana wakati wa uongozi wake, Rais Barack Obama amezungumzia kuhusu kuimarishwa uchumi wa Marekani, kupunguzwa shughuli za kijeshi nchini Afghanistan na Iraq, kupunguzwa kwa sehemu kubwa mtindo wa kutegemea mafuta kutoka nje na makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Wananchi washerehekea uamuzi wa korti kuhusu huduma za afya Obamacare
Wananchi washerehekea uamuzi wa korti kuhusu huduma za afya ObamacarePicha: Reuters/J. Roberts

ObamaCare ndio kipaumbele

Lakini mageuzi ya huduma za afya, yanayojulikana kama "Afordable Care Act" yaliyofikiwa mwaka 2010 na kupewa jina la ObamaCare, ambayo Donald Trump anadhamiria kubatilisha mara tu baada ya kuingia madarakani Januari 20, ndio yanayokamata nafasi ya mbele miongoni mwa mafanikio ya utawala wa Barack Obama.

Hata kabla ya kuondoka madarakni, Barack Obama ameanzisha juhudi za kuyanusuru mageuzi ya huduma ya afya. Jana alifanya ziara ya nadra katika bunge la Marekani Congress ili kuwagutua wafuasi wa chama cha Democrats kabla ya kile kinachotazamiwa kuwa "pambano la mwanzo kubwa" la rais mpya wa Marekani.

Ziara hiyo imetokea wakati mmoja na ile iliyofanywa na makamo mteule wa rais Mike Pence aliyekuja kuonana na wabunge wa chama chake cha Republican kinachodhibiti mabaraza yote mawili ya bunge.

"Kubatilishwa sheria ya bima ya afya au Obamacare ndio mada kuu katika ratiba ya bunge" amesema Mike Pence mwishoni mwa ziara hiyo.

Mwenyewe rais mteule, Donald Trump alionya hapo awali dhidi ya watu kufanya pupa, na kushauri kupitia mtandao wa kijamii Twitter "waiache Obamacare" iporomoke yenyewe.

Wabunge wa chama cha Democrats mbele ya jengo la Capitol Hills mjini Washington
Wabunge wa chama cha Democrats mbele ya jengo la Capitol Hills mjini Washington DC.Picha: Getty Images/A. Wong

 Utawala wa Obama umejitahidi kuondowa ukosefu wa usawa katika jamii

Katika risala yake, Barack Obama anasema Marekani imefanya kazi kubwa katika kupunguza hali ya kutokuwepo usawa katika jamii."

"Halitokua jambo la maana, kuwapokonya bima ya afya Wamarekani milioni 30, wengi wao ni wazungu na wanaotokea katika tabaka la waajiriwa, kuwapokonya nyongeza za mishahara kwa kazi ziada walizofanya wafanyakazi ambao wanastahiki, au kuzigeuza ziwe za kibinafsi huduma za afya na huduma za jamii na kuliachia upya soko la hisa, Wall Street lidhibiti hali ya mambo. Wamarekani wa tabaka la kati hawakuyapigia kura mambo hayo-amesema Rais Obama katika risala yake.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo