1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ataka ufafanuzi zaidi

12 Novemba 2009

Rais Barack Obama wa Marekani ambaye leo anaanza ziara ya bara la Asia, ametaka ufafanuzi zaidi kuhusiana na mapendekezo ya mbinu mpya katika vita vya Afghanistan.

https://p.dw.com/p/KUWA
Rais Obama katika kikao cha kujadili vita AfghanistanPicha: AP

Ikulu ya Marekani imesema Rais Obama alifafanua hayo katika kikao chake na maafisa wa juu ya usalama juu ya vita vya Afghanistan.

Rais Obama kwa mujibu wa taarifa ya White House, ametaka kwanza kujua,masuala mbalimbali kama vile uwajibikaji wa serikali ya Afghanistan katika kukabiliana na rushwa.

Pia alisema anaamini kuwa serikali ya Afghanistan itambue wazi kuwa kuwepo kwa majeshi ya Marekani nchini humo kuna mwisho wake.

Kikao hicho kiliwajumuisha, Waziri wa Ulinzi Roberts Gates, mwenyekiti wa jopo la wakuu wa majeshi ya Marekani, Admiral Mike Mullen, Jeneral David Petraus pamoja na mjumbe maalum wa Marekani nchini Pakistan na Afghanistan Richard Holbrooke.Pia kamanda wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan Jenerali Stanley McChrystal alishiriki kwa njia ya video moja kwa moja kutoka Afghanistan.

Akizungumza  mara baada ya kikao hicho Jenerali Petraus alisema.

General David Petraeus kurz vor seiner Anhörung vor dem US-Kongress
Jenerali David PetraeusPicha: AP

´´Tuko karibu kufikia uamuzi.Nadhani ni  suala la msingi kutilia maanani sababu ya vita vya Afghanistan ambayo ni kuhakikisha kuwa nchi hiyo haiwi tena maficho ya magaidi au pepo ya al Qaida na watu wenye msimamo wa siasa kali waliyofanya shambulizi la Sept 11´´

Kumekuwa na taarifa kuwa Rais Obama huenda akaridhia kuongezwa kwa wanajeshi zaidi nchini Afghanistan, kama ambavyo imependekezwa na makamanda wa kijeshi wa nchi hiyo.

Hata hivyo Rais Obama amekuwa na tahadhari ya hali ya juu katika kufikia uamuzi huo, mnamo kipindi hiki ambacho kimeshuhudia vifo vya wanajeshi wa Marekani katika vita hiyo vikiongezeka.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje  wa Marekani Jeneral Collins Powel akizungumza katika kituo cha radio nchini Marekani jana usiku alimtahadharisha Rais Obama juu ya uamuzi wa kuongeza askazi zaidi. ´´Hii ni ngumu sana.Huu ni uamuzi utakaokuwa na madhara kwa utawala wake.Kwa hiyo ndugu rais usikubali shinikizo kutoka kulia wala kushoto.Chukua muda zaidi kufikiri.Wewe ni Amiri jeshi mkuu na hilo ndilo ulilochaguliwa nalo´´

Katika hatua nyingine mjumbe maalum wa Marekani nchini Marekani , Karl Eikenberry amepinga hatua yoyote ya kuongezwa kwa wanajeshi zaidi nchini Afghanistan.

Gazeti la Washington Post limearifu kuwa Eikenberry ambaye Jenertalia mstaafu wa jeshi, pia ameelezea wa si wasi wake juu ya  mwenendo wa Rais Hamid Karzai aliyechaguliwa tena katika uchaguzi uliyogubikwa na vitendo vya hila.

Hata hivyo taarifa zinadokeza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Hillary Clinton, Waziri wa Ulinzi, Roberts Gates na Mwenyekiti wa wakuu wa majeshi ya nchi hiyo Admiral Mullen wanapendelea kuongezwa kwa wanajeshi elfu 30 zaidi nchini Afghanistan.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman