1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ataka kura juu ya umiliki wa silaha

Admin.WagnerD13 Februari 2013

Changamoto za kiuchumi zinazowakabili Wamarekani pamoja na suala la udhibiti wa silaha ni miongoni mwa mambo yaliyotawala kwenye hotuba ya Rais Barack Obama wa Marekani aliyoitoa mjini Washington.

https://p.dw.com/p/17dGk
GettyImages 161606978 President Barack Obama, flanked by Vice President Joe Biden and House Speaker John Boehner of Ohio, gestures during the State of the Union address before a joint session of Congress on Capitol Hill in Washington, Tuesday Feb. 12, 2013. AFP PHOTO / Pool / Charles Dharapak (Photo credit should read CHARLES DHARAPAK/AFP/Getty Images)
Obama Rede am 12.02.2013Picha: AFP/Getty Images

Obama amewataka watunga sheria wote nchini humo kuipigia kura miswada inayopendekeza sheria kali za udhibiti wa silaha ili kuyanusuru maisha ya raia wa taifa.

"Wanastahiki kura, Gab Gifford anastahili kura, familia za Newtown zinastahiki kura, familia za Aurora zinastahiki kura, familia ya Trey na watoto wawili na jamii nyingine zenye mashaka ambazo ziko hatarini kutokana na matumizi mabaya ya silaha wanastahiki kura", alisema Obama.

Kauli hiyo ya rais Obama ni miongoni mwa mada iliyozusha hisia ndani ya ukumbi aliotolea hotuba ambapo viongozi wa serikali, wanasiasa, wabunge, waathirika wa mashambulizi ya silaha pamoja na familia za merehemu waliokufa kutokana na kupigwa risasi wote walisimama huku baadhi yakibubujikwa na machozi.

Baraza la Kongresi katika hotuba Obama
Baraza la Kongresi katika hotuba ObamaPicha: Reuters

Obama aliwaambia wabunge wote kuwa anafahamu kwamba hiyo si mara ya kwanza kwa Marekani kuingia kwenye mjadala kuhusu kupunguza mauwaji ya kutumia silaha lakini akasema kuwa mara hii hali ni tofauti na kwamba kila pendekezo lililoletwa mbele yao linastahili kupigiwa kura. Obama alilitaka pia baraza la Kongresi kuchukua hatua ili kuzuia watu kununua silaha na kisha kuwauzia wahalifu.

Kiongozi huyo alisema kuwa wakuu wa polisi wanaomba msada wao ili waweze kuziondoa mitaani silaha za kivita na zile zenye uwezo wa kuuwa watu wengi kwa dakika chache kwa kuwa hata wao wamechoka kushambuliwa kwa risasi kila kukicha.

Chapuo la Obama kwa tabaka la kati

Kando na suala la umiliki silaha, uchumi na hali ya maisha ya Wamarekani ni masuala mengine yaliyozungumziwa katika hotuba hiyo. Obama alirejelea msimamo wake wa enzi za kampeni wa kutaka kuboresha maisha ya watu wa kipato cha kati huku akisisitiza juu ya kuboresha ujuzi na malipo mazuri.

Rais Barack Obama mwanzoni mwa hotuba yake
Rais Barack Obama mwanzoni mwa hotuba yakePicha: Reuters

"Wengi wetu tunakubali kupunguza nakisi ya bajeti ni lazima iwe sehemu ya ajenda yetu. Lakini hebu tuwe wazi, kupunguza nakisi ya bajeti pekee sio mpango wa kiuchumi. Uchumi unaokua na kutoa fursa nzuri za ajira kwa watu wa tabaka la kati ndio unaotakiwa kuwa nyota iongazayo juhudi zetu", alisema.

Kiongozi huyo alilitaka baraza la wawakilishi ambalo lina wingi wa wanasiasa kutoka chama cha Republican kuacha kuichezea nchi kwa kuingiza siasa kwenye suala nyeti la uchumi wa taifa.

Wanajeshi 34,000 wa Marekani kuondoka Afghanistan

Pamoja na mambo mengine ya ndani, aliutaja mpango wa kuondoa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan na kusema kuwa wanajeshi wapatao 34,000 wataondoka nchini humo mwanzoni mwa mwaka 2014.

Nchi hiyo bado iko katika mazungumzo juu ya mchango wake kwenye suala la amani na utulivu wa Afghanistan mara yakapoondoka majeshi ya jumuiya ya kujihami ya NATO yanayopambana na makundi ya kigaidi nchini humo.

Wanajeshi wa Marekani Afghanistan
Wanajeshi wa Marekani AfghanistanPicha: Reuters

Aidha rais huyo amezungumzia pia masuala ya biashara na kuweka wazi kuwa Marekani itafanya mazungumzo ya kina na Umoja wa Ulaya kuhusu biashara huria.

Kiongozi wa wabunge wa chama cha SPD cha Ujerumani Stein Meier amesema kuwa hotuba hiyo inaonyesha ni kiasi gani Obama analiwekea mkazo suala la ushirikiano wa kuchumi na Ulaya.

Mwandishi: Stumai George/Dpa/Afp/Reuters

Mhariri: Daniel Gakuba