1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama asisitiza Marekani imejizatiti kuzisaidia Aghanistan na Pakistan.

7 Mei 2009

Ni baada ya kukutana na marais Karzai na Zardari

https://p.dw.com/p/HlIa
Rais Obama akizungumza na waandishi habari Ikulu. Kulia ni rais Zardari wa Pakistan.Picha: AP

Rais Barack Obama wa Marekani, amezipongeza Pakistan na Afghanistan kwa kujizatiti kwao kuisaidia Marekani kupambana na magaidi walioweka ngome katika ardhi zao. Lakini pia alitoa tahadhari akisema mwendo wa kuelekea kwenye mafanikio ni wa pole pole na usio wa uhakika. Matamshi hayo yalitolewa mbele ya viongozi wa Pakistan na Aghanistan mjini washington wakati hali ikizidi kuwa tete nchini Pakistan.

Obama alikua amewaita marais wenzake Hamid Karzai wa Afghanistan na Asif Ali Zardari wa Pakistan mjini Washington jana,kuupa nguvu mpango wake mpya kwa nchi hizo mbili jirani, kila moja ikikabiliwa na matumizi ya nguvu na kitisho cha Taliban na kundi la Al Qaeda.

Obama alitamka " Ninafurahi kuona kwamba viongozi hawa waliochaguliwa wa Afghanistan na Pakistan, wanazingatia kikamilifu kitisho tunachokabiliana nacho na kusisitiza utajitolea kwao kupambana nacho."

Aidha kwa mujibu wa mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani James Jones, rais Obama alianza mkutano wake na rais Karzai kwa kuelezea masikitiko yake juu kuuawa kwa raia wasio na hatia katika hujuma za Marekani dhidi ya waasi

Wakati huo huo hali inazidi kuwa tete nchini Pakistan. Helikopta za kijeshi na ndege za kivita ziliendeleza mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa Kitaliban huku mashirika ya haki za kibinadamu yakitoa wasiwasi kuwa raia milioni moja wamekwama na wapo katika hali ya hatari.

Neue Militäroffensive gegen Taliban in Pakistan
Mwanajeshi wa Pakistan akipiga doria katika bonde la Swat.Picha: picture-alliance/ dpa

Pakistan inashinikizwa na Marekani kuwaangamiza wanamgambo wa kitaliban waliopo katika bonde la SWAT. Makubaliano ya amani kati ya Wataliban na Pakistan yalisambaratika wiki mbili zilizopita. Majeshi ya serikali yalizilenga ngome kuu za Taliban katika maeneo ya Malam, Jabba,Matta na Khawaza Khela.

Wachambuzi wanasema uamuzi wa Pakistan kukubali wakaazi milioni tatu wa jimbo la Swat kaskazini magharibi mwa nchi hiyo kuwa chini ya sharia za Kiislamu katika jitihada za kumaliza uasi wa Taliban sasa umo mashakani lakini Pakistan imesema utawala wa sheria utabakia kama ulivyo, kwani ni takwa halisi la wakaazi wa eneo hilo.

Katika tukio jengine linaloonekana kuwa ni pigo, mtoto mkubwa wa kiume wa kiongozi wa kidini aliyesaini makubaliano hayo na serikali aliuwawa, pale ndege za kivita zilipolishambulia kwa mabomu eneo la La Qila.

Maulana Kifayatullah mwenye umri wa miaka 50 na mtoto mkubwa miongoni mwa watoto 12 wakiume wa Sheikh Sufi Mohammad aliuwawa na shemeji yake kujeruhiwa miguu.

Flucht aus dem Swat-Tal
Wakaazi wa Mingora mji mkuu wa Swat wakijaribu kuuhama mji huo.Picha: AP

Kamishna wa umoja wa mataifa anayehusika na wakimbizi Antonio Guterres amesema na wasi wasi juu ya Wapakistan waliotawanyika na baadhi ya wakimbizi 20.000 walio orodheshwa kutoka Afghanistan na kwamba shirika hilo linaimarisha misaada kwa watu hao.

Msemaji wa Taliban Muslim Khan kwa upande amedai kwamba licha ya hujuma za jeshi la serikali, wao bado wanaidhibiti 90 asili mia ya ardhi ya mkoa huo wa SWAT.

Mwandishi:M.Abdul-Rahman/AFPE

Mhariri: