1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama asema vyombo vya Usalama nchini humo vilijua jaribio la kulipua ndege.

Halima Nyanza6 Januari 2010

Rais Barack Obama ameelezea kukasirishwa kwake na kile alichokielezea kama uzembe mkubwa uliofanywa na mashirika ya upelelezi kushindwa kuzuia jaribio la kuripua ndege ya Marekani wakati wa Krismas.

https://p.dw.com/p/LLxO
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: AP

''..Nimewaita viongozi hawa Ikulu kwa sababu tunakabiliwa na changamoto kubwa ya dharura, kama tulivyoona wakati wa sikukuu ya Krismas, Al Qaeda na washirika wake wenye msimamo mkali za kufanya kila liwezekanalo kuwaangamiza Wamarekani. Tumeamua sio tu kuzuia mipango hiyo, lakini kuivunja, kuiondoa na kuivunja mitandao yao mara moja...'', alisema Rais Obama.

Ameyasema hayo kwa sauti iliyojaa msisitizo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari mara baada ya kukutana kwa takriban muda wa saa mbili na wakuu wa vyombo vya Usalama nchini humo.

Amesema mashirika ya kijasusi nchini humo yalikuwa na taarifa za kutosha kuweza kugundua njama za kuripua ndege ya Marekani iliyokuwa ikitokea Amsterdam kwenda Detroit, lakini walishindwa kufanikisha kuzuia jaribio hilo.

Vyombo vya usalama vilikuwa na taarifa ya mashambulio: Mashirika ya Kijasusi ya Marekani na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya nchi hiyo zilikuwa na taarifa kuhusiana na mtu aliyefanya jaribio hilo, raia wa Nigeria, Umar Farouk Abdulmutallab, lakini kamwe hawakukusanya taarifa kuweza kumuweka katika orodha ya wale wasiotakiwa kusafiri kuingia nchini humo.

Umar Farouk Abdulmutallab
Umar Farouk Abdulmutallab, Vyombo vya usalama vya Marekani vilijua njama zake.Picha: AP

Rais Obama amekiri kwamba upelelezi una mapungufu, lakini haikubaliki kusema kwamba wapelelezi hawakuwa na uwezo wa kutosha.

Aidha amewaeleza washauri wake hao wa masuala ya Usalama kwamba anataka uchunguzi wa awali kukamilishwa wiki hii na taarifa kamili juu ya kipi kilichosababisha mambo kwenda kombo.

Amesisitiza kuwa maisha ya Wamarekani yako hatarini hivyo wanapaswa kuimarisha juhudi zao kiusalama na kwa haraka ili kosa kama hilo lisijirudie na kuweza pia kuzuia mashambulio mengi yatakayopangwa kufanywa baadaye.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini humo, Dennis Blair, amesema wamepata ujumbe uliotolewa na Rais na kwamba wako katika harakati kukabiliana na changamoto hizo mpya.

Katika taarifa yake aliyoitoa, mkurugenzi huyo amesema mfumo uliokuwepo haukuweza kumkamata Mnigeria huyo na kumzuia kupanda ndege na kuingia Marekani.

Amesema vitisho vinaendelea na hivyo wanahitaji kuimarisha uwezo wao kupambana na hali hiyo na kuwalinda Wamarekani.

Nacho chama cha upinzani nchini humo cha Republican kimeikosoa serikali inayoongozwa na chama cha Democratic kwa kuwa dhaifu na kushindwa kupambana na ugaidi.

Aidha Chama hicho cha upinzani kinatarajia kutumia udhaifu huo kupata kura nyingi katika uchaguzi ujao wa mwezi Novemba.

Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri: Othman, Miraji