1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aongoza kura za maoni

19 Septemba 2012

Kura za maoni nchini Marekani zinamuonesha Rais Barack Obama akiongoza mbele ya mshindani wake mkuu, Mitt Romney, huku wakosoaji wakimsakama Romney kwa kauli zilizowakasirisha wapiga kura juu ya sera ya afya ya Obama.

https://p.dw.com/p/16BPj
Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: dapd

Hata kama maoni haya ya wapiga kura wa Marekani yalikusanywa kabla ya kutolewa kwa vidio ya siri inayomuonesha Romney akiwaambia wafadhili wake matajiri kwamba asilimia 47 ya wapiga kura wa Marekani ni wategemezi wa serikali ambao watampigia kura Obama kuendelea kupata ruzuku ya serikali na kwamba hajali kuhusu hao, tayari inaonekana kwamba Romney amekalia kuti kavu.

Rais Obama ameiita kauli hiyo kuwa ni ya kiongozi asiyewajibika kwa umma. "Ninapokuwa ninatembelea sehemu mbalimbali kwenye nchi yetu, nakutana na watu ambao wanajituma sana na ambao wanajali kuhusu nchi hii. Na matarajio yangu ni kwamba kama unataka kuwa rais, unalazimika kuwa tayari kufanya kazi ajili ya kila mtu na sio baadhi yao tu." Amesema Rais Obama.

Hadi sasa Romney hajaikanusha wala kuomba radhi kwa kauli hiyo, badala yake amesema kwamba ni maoni yake ambayo yanaonesha tafauti ya kimsingi iliyopo kati yake na Obama.

Kwa mujibu wa matokeo ya kura ya maoni yaliyochapishwa leo kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Quinnipiac, gazeti la New York Times na kituo cha televisheni cha CBS News, Rais Barack Obama anaongoza katika majimbo matatu muhimu ya Virginia, Wisconsin na Colorado na majimbo mengine yote muhimu yenye wapiga kura waliokuwa hawajaamua.

Obama yuko mbele ya Romney

Obama amemtangulia Romney kwa asilimia 51 kwa 45 katika jimbo la Wisconsin, ambako ndiko nyumbani kwa mgombea mwenza wa Romney, Paul Ryan, wakati katika jimbo la Virginia akiongoza kwa 50 kati ya 46 za Romney na 48 kwa 47 katika jimbo la magharibi la Colorado. Obama alishinda majimbo yote matatu mwaka 2008, alipokuwa mgombe wa kwanza Democrats kushinda Virginia tangu mwaka 1964.

Rais Barack Obama na timu yake baada ya kusaini sheria ya mageuzi ya kifedha.
Rais Barack Obama na timu yake baada ya kusaini sheria ya mageuzi ya kifedha.Picha: AP

Katika eneo la uchumi, wagombea hao wawili wanachuana vikali katika majimbo yote matatu, Obama akiongoza kwa asilimia 49 kwa 46 za Romney kwenye jimbo la Winsconsin, ambapo katika eneo la kimataifa, Obama yuko mbele kwa asilimia 50 dhidi ya 43 za Romney kwenye jimbo la Colorado na 53 dhidi ya 42 kwenye jimbo la Virginia. Obama pia ameongoza kwenye eneo la vita dhidi ya ugaidi, ambapo matokeo yanamuonesha akiwa na asilimia 50 dhidi ya 41 katika jimbo la Colorado.

Matokeo haya yalikusanywa kati ya tarehe 11 na 17 Septemba, katika wakati ambapo maandamano dhidi ya filamu inayoukashifu Uislamu yalipokuwa yamepamba moto katika sehemu kadhaa duniani, ikiwemo nchini Libya, ambako balozi wa Marekani na Wamarekani wengine waliuawa mjini Benghazi.

Romney alikumbana na lawama kali baada ya kumtuhumu Obama kwa kuwaonea huruma waandamanaji katika kauli aliyoitoa masaa 11 baada ya balozi huyo kuuawa. Wakosoaji wake, wakiwamo wa wahafidhina wengi, walimtuhumu Romney kwa kumkashifu rais kisiasa katika wakati wa mgogoro wa kimataifa kama huo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters/AP
Mhariri: Saumu Yusuf