Obama amshinda Hilary Clinton huko South Carolina
28 Januari 2008Matumaini ya seneta Barack Obama kugombea urais wa Marekani yameongezeka baada ya kiongozi huyo kumshinda mpinzani wake Hilary Clinton katika uchaguzi wa jimbo la South Carolina.
Juhudu za Obama kushinda nafasi ya kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic zinazidi kupamba moto huku mbunge mashuhuri wa chama cha Democratic, wa jimbo la Massachusetts, Ted Kennedy, akijiandaa kumuidhinisha rasmi kama mgombea wa chama hicho katika uchaguzi ujao nchini Marekani.
Mwanasiasa huyo wa familia ya Kennedy amejiunga na mpwa wake Caroline Kennedy ambaye pia amemuidhinisha Barack Obama, akisema anamkumbusha babake, rais wa zamani wa Marekani, John F Kennedy.
Hatua ya Ted Kennedy ya kumuunga mkono Barack Obama haikutarajiwa na ni pigo kubwa kwa Hilary Clinton. Seneta Kennedy amechukua uamuzi huo na kukataa mwito wa rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, kumtaka amuunge mkono seneta Hilary Clinton.