Obama ampiku Romney mdahalo wa televisheni
23 Oktoba 2012Safari hii, wachambuzi wanasema kwamba mpira ulikuwa unachezwa uwanjani kwa Rais Obama - siasa za kimataifa - na hivyo alitumia vizuri ujuzi wake kwenye eneo hilo kuponda kile kinachoonekana kama uelewa mdogo wa Romney linapohusika suala la siasa za nje.
"Gavana Romney, nimefurahi kwamba unatambua kwamba al-Qaida ni tishio kwa sababu miezi michache iliyopita ulipoulizwa ni kipi kitisho kikubwa duniani kwa Marekani, ulisema Urusi, ilhali Vita Baridi vilimalizika tangu miaka 20 iliyopita. Linapokuja suala la sera za nje, unaonekana kurudisha siasa za miaka ya 1980, kama vile ambavyo una sera za kijamii za mwaka 1950 na za kiuchumi za mwaka 1920. Unasema hupendelei kuigiza kilichotokea Iraq, lakini wiki chache zilizopita ulisema unafikiria tuongeze wanajeshi zaidi nchini Iraq." Obama alimdhihaki Romney.
Pakiwa pamebakia wiki mbili tu kabla ya Siku ya Uchaguzi, Romney aliutumia mdahalo wa jana kushadidia hoja yake kwamba Obama ameufuja uchumi wa Marekani
"Ili tuweze kuendeleza misingi hiyo ya amani, tunahitajika kuwa na nguvu, na hilo linaanza na uchumi imara hapa kwetu, na bahati mbaya uchumi si imara kiasi hicho. Pale rais wa Iraq- samahani- rais wa Iran, Ahmedinejad, anaposema kwamba deni letu linatufanya tusiwe tena taifa kubwa, hilo ni jambo la kutisha. Mkuu wa zamani wa jeshi, Admirali Mullen, alisema kwamba deni letu ndicho kitisho kikubwa cha usalama wa taifa. Tumeudhoofisha uchumi wetu." Alisema Romney.
Mchuano mkali
Wakiwa wanachuana vikali, hakuna hata mmoja kati yao aliyeweza kumtoa mwenzake nje ya ulingo haraka, wakati wakilumbana kuhusiana na masuala ya Israel, Iran, Urusi, na ukubwa wa jeshi la Marekani, katika mdahalo huo uliofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Lynn, Boca Raton.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni yaliyotangazwa baada ya mdahalo huo, yamemuonesha Obama akiongoza, ingawa asilimia 60 ya waliotuma maoni yao kwenye kituo cha CNN, walisema Gavana Romney ana uwezo wa kuwa amiri jeshi mkuu wa majeshi, akitimiza jukumu lililowekwa na wasaidizi wake. CNN imempa Obama asilimia 8 mbele ya Romney.
Kura ya maoni ya kituo cha CBS inaonesha kuwa asilimia 53 ya watu wanaamini kuwa Obama alishinda mdahalo wa jana, ikilinganishwa na asilimia 23 ya Romney, huku asilimia 24 wakisema wametoka suluhu.
Kwa kuwa siasa za nje ni kipaumbele cha chini katika kampeni iliyojikita kwenye uchumi, bado si wazi ikiwa mdahalo huu utakuwa na athari gani kwenye kinyang'anyiro hicho cha urais. Wachangiaji maoni kupitia kituo cha CNN, walionekana kugawika juu ya suala ikiwa mdahalo huo ungeliathiri kura zao hapo tarehe 6 Novemba.
Hata hivyo, picha hii ya Boca Raton ilikuwa ni moja ya nafasi za mwisho mwisho kabisa kwa wagombea wote wawili kuwanasihi mamilioni ya wapiga kura waliokuwa wakiifuatilia kupitia televisheni zao, na ambapo Obama ametajwa kujidhihirisha mtundu zaidi ya Romney.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf