Obama amemshinda Clinton katika jimbo la Maine
11 Februari 2008Seneta Barack Obama wa jimbo la Illinois nchini Marekani amemshinda mpinzani wake wa chama cha Democratic, Hillary Clinton, kwenye uchaguzi uliofanyika katika jimbo la Maine, kumtafuta mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama hicho.
Ushindi wa Obama katika jimbo hilo unamuongezea nguvu mwanasiasa huyo katika juhudi za kushinda uteuzi wa chama kugombea urais wa Marekani.
Jumamosi iliyopita Obama alimshinda Hillary Clinton katika majimo ya Louisiana, Nebraska, Washington na visiwa vya Virgin.
Hata hivyo Clinton ametoa mwito wa kutaka achaguliwe kuwania urais wa Marekani.
Ushindi wa Obama katika chaguzi zote tano za mwishoni mwa juma zimemfanya akaribiane sana na Clinton katika kinyang´anyiro cha kuwania idadi ya wajumbe walio na jukumu la kumchagua mgombea urais katika mkutano wa chama utakaofanyika baadaye mwaka huu.