Obama alihutubia Baraza kuu la Umoja wa mataifa.
23 Septemba 2009Baraza kuu la umoja wa mataifa limeanza kikao chake cha kila mwaka mjini New York leo, huku macho yote akikodolewa Rais wa Marekani Barack Obama aliyelihutubia baraza hilo kwa mara ya kwanza muda mfupi uliopita.
Katika hotuba yake Rais Obama alisema dunia inahitaji kushirikiana pamoja chini ya misingi ya kuheshimiana na kuvumiliana. akasema wakati wa hotuba tu umekwisha badala yake hatua za kivitendo . Kiongozi huyo wa Marekani alitaja juu ya hatua zilizochukuliwa na utawala wake, ikiwa ni pamoja na kupinga mateso, kulifunga gereza la Guantanamo na kutangaza ratiba ya kuondoa wanajeshi wake nchini Irak.
Kiongozi huyo wa Marekani aliyekua akilihutubia baraza kuu la umoja wa mataifa kwa mara ya kwanza aliwaambia viongozi wenzake kwamba Marekani haiwezi kutatua matatizo yote ya dunia peke yake na badala yake panahitajika ushirikiano zaidi baina ya mataifa kuyakabili matatizo hayo kwa pamoja.
Rais Obama akazungumzia pia haja ya kuzuwia kusambaa kwa silaha za nyuklia . Akasema nchi yake itaendeleza mazungumzo na Urusi kupunguza silaha hizo. Akizungumzia migogoro duniani alisema Marekani itaendeleza juhudi za kupatikana amani kati ya Israel na Wapalestina na haja ya mataifa mawili Israel na Palestina kuishi pamoja na pia amani ya mashariki ya kati kwa jumla .Pia akataja juu ya haja ya kupatikana amani huko Darfur, alakini dunia kwa jumla lazima iamuwe kama kweli imejizatiti kuishi kwa amani.
Hotuba yake pia iligusia juu ya ongezeko la ujoto duniani kufuatia mabadiliko ya hali ya hewa na suala la umaskini na kuongezeka kwa maradhi . Obama akaonya juu ya kitisho kinachoukabili ulimwengu pindi jumuiya ya kimataifa haitashikamana kukabiliana na matatizo hayo.
Hapo awali kikao cha baraza hilo kilifunguliwa na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon, ambaye alitoa wito mbele ya zaidi ya viongozi 120 akiwataka kuchukua hatua ya dhati na ya pamoja,kuzuwia mabadiliko ya hali ya hewa, kupambana na umasikini duniani na kushinikiza juu ya kupunguzwa silaha za nukliya.Aidha alitoa pia wito wa kumalizwa migogoro duniani,"Tunataka kumaliza umwagaji damu katika Gaza, masuala ya haki na uwajibikaji yanapaswa kushughulikiwa, lazima kufufua mazungumzo juu ya kuwepokwa dola mbili na utaratibu madhubuti wa amani ya Mashariki ya kati."
Kikao cha mwaka huu pia kinahudhuriwa na viongozi wawili ambao kuwepo kawao kumegonga vichwa vya habari. Hao ni rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran na Kiongozi wa Libya ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika Kanali Muammar Gaddafi. Baadhi ya wajumbe wa nchi za magharibi ikiwemo Ujerumani wameshtamka kwamba wataondoka kikaoni pindi wakati wa hotuaba yake Rais Ahmadinajed atatoa matamshi ya kukana maangamizi makubwa ya Wayahudi wakati wa vita vya pili vya dunia au matamshi yanayoashiria chuki dhidi ya Wayahudi.
Kwa upande wa Gaddafi atalihutubia baraza kuu kwa mara ya kwanza .Kiongozi habari tayari amekua kivutio kutokana na viroja vinavyohusiana na kuwepo kwake. Kiti chake mkutanoni kimeandikwa " Tuko hapa", na kwa mujibu wa mjumbe mmoja wa Libya maneno hayo yameandikwa kwa lugha ya Kiingereza na Kiarabu.
Tayari jana kulizuka utata mwengine, wakati kanali Gaddafi alipotaka ajengewe hema katika mji wa Bedford na kuwa maskani yake , lakini maafiwa wa mji huo wakazuwia hatua hiyo wakisema inakwenda kinyume na sheria za mji huo.
Hapo kabla maafisa wa Gaaddafi walitaka kujenga hema hilo katika bustani kuu ya jiji la New York na paia katika eneo la ubalozi wa Libya katika kitongoji cha New Jersey lakini matamkwa yote mawili yakazuiwa. Hadi sasa haijulikani Kiongozi huyo wa Libya atakaa wapi wakati wa ziara hii ya Marekani,aya kwanza tangu 1969 alipotwaa madaraka katika mapinduzi yaliomuangusha Mfalme Idris 1969.
Mwandsihi: M. Abdul-Rahman /rtr
Mahariri:Thelma Mwadzaya