Obama akutana na wanahabari kwa mara ya mwisho
19 Januari 2017Katika tukio hilo la mwisho kwa Rais Obama kabla ya rais mteule Donald Trump kuchukua madaraka hapo kesho, katika masuala ya kimataifa, kiongozi huyo amekiri kwamba ana wasiwasi kuhusu suluhisho la mataifa mawili kutokana na mzozo unaoendelea kati ya Israel na Palestina, ikiwemo ujenzi wa makaazi ya Walowezi katika Ukingo wa Magharibi.
''Nina wasiwasi kuhusu pande zote mbili kwa sababu nadhani hali iliyopo ni endelevu. Hali ni hatari kwa Israel, suala hilo ni hatari kwa Wapalestina, hali ni mbaya katika ukanda wa Mashariki ya Kati na pia ni hatari kwa usalama wa taifa la Marekani,'' alisema Obama
Rais Obama amesema serikali yake haikulizuia azimio la hivi karibuni la Umoja wa Mataifa kuhusu shughuli za ujenzi wa makazi ya Walowezi katika ardhi ya Wapalestina inayokaliwa na Israel, kwa sababu iliona kwamba suluhisho la mataifa mawili ndiyo njia bora ya kupatikana kwa amani.
Amebainisha kuwa hataki kutabiri kile kinachoweza kutokea, akimaanisha dhahiri mpango wa Trump wa kutaka kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem. Amemuonya Trump dhidi ya kuchukua hatua za upande mmoja kuhusu mji wa Jerusalem.
Uhuru wa vyombo vya habari
Obama pia amezungumzia kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na kusema kwamba demokrasia haiwezi kufanikiwa vizuri, kama hakuna raia ambao wamepata habari vizuri na kulikuwa na kazi muhimu ya kuanzisha misingi ya ukweli na ushahidi. Amebainisha kuwa uhuru wa habari ni sehemu ya jinsi Marekani inavyofanya kazi kama taifa.
Ama kwa upande mwingine Rais Obama ametetea maamuzi yake ya mwisho aliyochukua akiwa madarakani, ukiwemo uamuzi wa kupunguza kifungo cha miaka 35 jela dhidi ya Chelsea Manning, aliyevujisha maelfu ya nyaraka za siri kwa mtandao wa kufichua siri wa Wikileaks. Amesema Manning alifikishwa mahakamani na kujutia makosa yake aliyoyafanya mwaka 2010.
Amesema Manning aliyekuwa mchambuzi wa masuala ya kijasusi wa jeshi, ametumikia vizuri kifungo chake gerezani na atatumika kama njia ya kuzuia mtu yeyote kufikiria kufanya kitendo kama hicho. Obama amesema ameridhika kwamba haki imefanya kazi vizuri.
Rais Obama pia amezungumzia maisha yake baada ya kuondoka madarakani, akisema atatumia muda mwingi kwa ajili yake mwenyewe pamoja na familia yake. Obama pia amethibitisha kuwa atahudhuria sherehe za kuapishwa Trump, tofauti na ilivyo kwa baadhi ya wanachama wenzake wa Democratic.
Mkutano wa jana na waandishi wa habari ulikuwa wa 39 akiwa mwenyewe, wa 21 akiwa katika chumba cha mikutano cha habari cha Ikulu ya White House na wa 224 kwa ujumla wa mikutano yote ya waandishi wa habari.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, DW, AFP
Mhariri: Idd Ssessanga