1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama Terrorbekämpfung Bilanz

Josephat Nyiro Charo19 Januari 2010

Ahadi zake nyingi ni ngoma kuzitimiza

https://p.dw.com/p/Lb0l
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: AP

Kufungwa kwa jela ya Guantanamo na kuondokana na sera za kutatanisha za utawala wa rais wa zamani wa Marekani, George W Bush katika kupambana na ugaidi, ni miongoni mwa ahadi alizozitoa rais wa sasa wa Marekani, Barack Obama wakati alipoingia madarakani. Ukweli lakini ni kwamba rais Obama, mtu anayebeba matumaini wengi ulimwenguni, aliahidi mambo mengi mno kupita yale ambayo angeweza kuyatimiza.

Matarajio yalikuwa makubwa mno. Kama watu wengi katika sehemu mbalimbali za ulimwengu walivyotumai, Rais Obama, angeigeuza Marekani katika vita vyake dhidi ya ugaidi kuwa taifa linaloongoza katika kutetea na kulinda haki. Visa vya mateso dhidi ya wafungwa na magereza ya kuzuia wafungwa ni mambo ambayo yalimtia ila rais wa zamani, George W Bush na kutia doa heba ya Marekani.

Rais Obama alijua kilichotarajiwa kutoka kwake na akatangaza kwa wakati muafaka kufungwa kwa jela ya Guantanamo. Lakini mwaka mmoja tangu kuingia madarakani, jela ya Guantanamo bado ingaliko na pia katika maswala mengine kuhusu vita dhidi ya ugaidi kiongozi huyo mahiri katika ikulu ya Marekani ameuona ukweli halisi wa mambo.

Siku ya Krismasi mwaka jana 2009 raia wa Nigeria ambaye ana mafungamano na kundi la al Qaeda, alikaribia kufaulu kuilipua ndege ya abiria ya Marekani ingawa vyombo vya usalama vya Marekani vilikuwa na habari kuhusu njama yake hiyo. Yemen nayo imeendelea kuwa ngome ya magaidi wa kiislamu na inaonekana wafungwa wa zamani kutoka jela ya Guantanamo waimeifanya Yemen kuwa maficho yao.

Sasa utawala wa rais Obama unajaribu kuwahamisha wafungwa kutoka jela ya Guantanamo nchini Cuba hadi Tomson, Illinois katika ardhi ya Marekani. Lakini ikiwa huko pia wafungwa wataendelea kuzuiliwa bila kufunguliwa mashtaka mahakamani, bado kutakosekana haki kwao, kwa sababu kufikia sasa rais Obama hajafaulu kuunda mahakama za kijeshi zilizozusha utata.

Rais Obama alijipatia sifa kubwa wakati aliporuhusu siri za rais aliyemtangulia George W Bush katika vita vya kupambana na ugaidi ziwekwe wazi hadharani. Katika swala hili rais Obama alitaka kwa haraka kuwepo na uwezo unaotakikana. Hata hivyo ukweli kwamba kufikia sasa hakuna afisa yeyote wa idara ya ujasusi au utawala wa rais Bush aliyechukuliwa hatua za kisheria kwa ukiukaji wa haki za binadamu, ni jambo ambalo bado lipo pembeni.

Jambo zuri la kutia moyo ambalo rais Obama amefaulu kulifanya katika kipindi hiki cha mwaka mmoja ni kufunga magereza yote ya siri ya shirika la ujasusi la Marekani, CIA na kuwahamisha washukiwa wa mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001 mjini Washington na New York katika magareza ya Marekani. Rais Obama katika vita dhidi ya ugaidi amerithi mlima mkubwa wa matatizo kutoka kwa utawala wa rais George W Bush.

Rais Obama amefaulu kuchukua hatua ya mwanzo, lakini hata hivyo mengi hajayafanikisha. Kuna mambo chungu nzima anayohitaji kuyakamilisha na washirika wake wanatakiwa kumsaidia sio tu kutoa ushauri na maonyo bali pia kutoa msaada muhimu anaouhitaji kama vile kukubali kuwachukua wafungwa kutoka jela ya Guantanamo.

Mwandishi: Daniel Scheschkewitz/Charo/ZPR

Mhariri: Othman Miraji