Obama aja juu katika mdahalo wa pili
17 Oktoba 2012Obama ameonekana kuzinduka kutokana na jinamizi lililomfanya aonekane mnyonge katika mdahalo wa kwanza uliofanyika mjini Denver mwezi uliopita, na maoni ya wachambuzi wengi ni kwamba ametawala jukwaa katika mdahalo wa pili, ambao umemalizika alfajiri ya leo ( 17.10.2012) kwa saa za Afrika ya mashariki. Kura za maoni zilizochapishwa na kituo cha televisheni cha CNN ambacho kimeendesha mdahalo huo, zimeonyesha kwamba Rais Obama ameibuka kifua mbele dhidi ya Gavana Romney ambaye ametetereka.
Mdahalo ulikuwa mkali, wagombea wakikabiliana ana kwa ana na kubadilishana maneno makali, huku kila mmoja akinuia kumuonyesha mpinzani wake kama mtu asiyefaa kuiongoza Marekani.
Kutoana kimasomaso
Rais Obama alimuangalia usoni na kumnyoshea kidole Romney, akijibu tuhuma za mgombea huyo wa chama cha Republican kwamba Obama na utawala wake walishindwa kuchukua hatua mwafaka kukabiliana na mashambulizi kwenye ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya, ambayo yalimuuwa balozi na raia wengine wanne wa Marekani.
''Madai yoyote kwamba mtu yeyote katika timu yangu, iwe waziri wa mambo ya nchi za nje, au balozi kwenye Umoja wa Mataifa, anaweza kutumia vifo vya watu wetu wanne kisiasa, ni uchokozi. Hayo siyo tunayofanya, hayo siyo ninayoyafanya kama rais na jemadari wa majeshi''. Alisema kwa ukali rais Obama.
Wa-Republican walitaka kuyatumia mashambulizi ya Benghazi kuzitia doa sifa alizopata Rais Obama katika masuala ya usalama na sera za nchi za nje.
Romney alijaribu kujipanga upya kwa kumshutumu Obama kutosema kwa wakati unaofaa kwamba mashambulizi yale yalikuwa tendo la kigaidi, lakini Obama alimpa changamoto ya kusoma hotuba aliyoitoa mara tu baada ya mashambulizi, na aliungwa mkono na mwongozaji wa mdahalo, Candy Crowly.
Romney ajibu mapigo
Wakati ambapo Romney alimbana pumzi rais Obama ni pale alipotoa shutuma kali akielezea jinsi rais huyo alivyoshindwa kufufua uchumi na kuunda nafasi za kazi kama alivyoahidi wakati aliposhinda muhula wa kwanza wa miaka minne.
Romney alisema, ''Alipochukua madaraka asilimia 7.8 ya wamarekani hawakuwa na ajira, wasio kuwa na ajira leo hii ni hao hao asilimia 7.8, lakini ukitilia maanani watu walitoka katika kundi la wafanyakazi, itakuwa asilimia 10.7. Hatujawa na maendeleo yanayowezesha kuwarudisha watu kazini''
Ahueni kwa upande wa Obama
Wachambuzi wanasema matokeo ya mdahalo wa leo yatawakatisha tamaa wa Republican ambao walitaka mgombea wao ammalize kabisa rais Obama, na kwa upande mwingine utashangiliwa na wa Democrats ambao wanaamini kwamba mgombea wao amepata msukumo mpya.
John Pitney ambaye ni profesa wa masomo ya siasa kwenye chuo kikuu cha Claremont McKenna, amesema usiku wa leo ulikuwa bora kwa Obama, ukilinganishwa na ule wa mjini Denver.
Mdahalo huu umefanyika zikisalia wiki tatu tu kabla ya uchaguzi wa mwezi Novemba. Mdahalo wa tatu na wa mwisho utafanyika tarehe 22 mwezi huu huko Boica Raton, Florida.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/RTRE
Mhariri:Yusuf Saumu